Mafanikio ya Misri katika Sekta ya Uchumi

Imeandikwa na: Menna Alla Ashraf Sayed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika miaka ya hivi karibuni, Misri imepata maendeleo makubwa ya kiuchumi kutokana na utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya kiuchumi wa kina na wa kisasa, kwa ushirikiano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pamoja na washirika wengine wa maendeleo. Serikali ya Misri ililenga kufanikisha uthabiti wa kifedha, kuboresha mazingira ya uwekezaji, na kukuza sekta za uzalishaji, sambamba na kuwekeza katika miradi mikubwa ya kitaifa.
Kuachia thamani ya sarafu huru mnamo mwaka 2016 kulikuwa hatua muhimu sana, kwani kuliimarisha imani katika uchumi wa Misri, kuongeza mitaji ya kigeni, na kuboresha mizania ya biashara. Vilevile, serikali ilitekeleza sera za kifedha zenye lengo la kupunguza nakisi ya bajeti na kushusha deni la umma hadi viwango endelevu.
Katika sekta ya nishati, Misri imejigeuza kuwa kitovu cha nishati kikanda baada ya kujitosheleza kwa gesi asilia na kuanza kuuza nje. Ugunduzi wa visima vikubwa kama vile "Zohr" umechangia sana mafanikio haya. Miradi ya nishati mbadala, kama vile kituo cha umeme wa jua cha Benban, mojawapo ya vikubwa zaidi duniani, imeongeza uzalishaji wa nishati safi.
Sekta ya miundombinu imepiga hatua kubwa, ikijumuisha ujenzi wa maelfu ya kilomita za barabara mpya, maboresho ya reli, na kuanzishwa kwa miji ya kisasa kama vile Mji Mkuu Mpya wa Utawala na New Alamein. Miradi hii inalenga kupunguza msongamano wa watu jijini Kairo, kuvutia uwekezaji mpya, na kutoa ajira kwa vijana.
Sekta ya utalii pia imeimarika sana baada ya kipindi cha kushuka, kwa msaada wa miradi mikubwa kama vile Jumba la Makumbusho Kuu la Misri, mojawapo ya makumbusho makubwa zaidi ya kale duniani, pamoja na kuboresha maeneo ya kitalii kama Hurghada na Sharm El-Sheikh, jambo lililochangia kuongeza idadi ya watalii.
Maendeleo ya kijamii yamepewa kipaumbele, kwa kuzindua mipango ya msaada wa kifedha kama vile Takaful na Karama, na kupanua huduma ya bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote.
Aidha, serikali imeweka mkazo mkubwa katika kusaidia biashara ndogo na za kati, na kuunda mazingira rafiki kwa ubunifu na ujasiriamali.
Shukrani kwa mageuzi haya, uchumi wa Misri umeweza kustahimili misukosuko mikubwa ya dunia, kama vile janga la COVID-19 na migogoro ya kiuchumi ya kimataifa, huku ukiendelea kukua kwa viwango chanya ikilinganishwa na mataifa mengine mengi.
Misri inaendelea na safari yake ya kujenga uchumi wenye nguvu, unaotegemea teknolojia, ubunifu, na utofauti wa vyanzo vya mapato, ili kufanikisha ndoto za vizazi vijavyo.