DARAJA LA JPM LIMEONGEZA FURSA ZA UTALII NA BIASHARA

DARAJA LA JPM LIMEONGEZA FURSA ZA UTALII NA BIASHARA
DARAJA LA JPM LIMEONGEZA FURSA ZA UTALII NA BIASHARA

Imeandikwa na: Evodius Oscar

Ziwa Victoria ni miongoni mwa maziwa makubwa na marefu zaidi nchini Tanzania na barani Afrika. Ukilitaja ziwa hili, huwezi kuacha kuitaja Tanzania, licha ya vivutio vingi vya utalii, imeyokuwa sehemu yenye fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wake na wageni kutoka mataifa mbalimbali. Ziwa hili linaunganisha nchi tatu: Tanzania, Kenya na Uganda.

Kutokana na changamoto ya idadi kubwa ya watu kushindwa kufikia fursa za kibiashara zilizoizunguka, mnamo mwaka 2019 Serikali ilianzisha mpango wa ujenzi wa Daraja la JPM. Mpango huu ulizinduliwa katika awamu ya tano ya uongozi wa hayati Rais John Pombe Magufuli. Daraja hili lina urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.4, likiwa na njia nne za magari na njia za dharura kwa watembea kwa miguu.

Daraja hili, ambalo sasa ni kivutio kikubwa cha kipekee Afrika Mashariki, limejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700 za Kitanzania, zikigharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Limesaidia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa biashara ya samaki, kilimo, na madini, na kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa. Awali, watu walisafiri majini kwa zaidi ya dakika 30, lakini sasa safari huchukua dakika nne hadi tano pekee.

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi Daraja la JPM mnamo tarehe 19 Juni mwaka huu akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine, tukio ambalo lilikuwa alama kubwa ya maendeleo ya miundombinu nchini Tanzania.
Daraja hili ndilo refu zaidi Afrika Mashariki na la sita kwa urefu barani Afrika, likifuatiwa na madaraja makubwa nchini Misri na Nigeria. Limeimarisha mtandao wa usafiri ndani ya Kanda ya Ziwa na kwa nchi jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Daraja la JPM Kigongo–Busisi limekuwa sasa nembo ya utalii na maendeleo kwa Taifa la Tanzania, likionesha ishara ya kujitegemea, kukuza uchumi na kuwaunganisha wananchi kwa urahisi, huku likibadilisha maisha ya watu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.