Juhudi za Misri katika Kuwezesha Wanawake

Imeandikwa na: Malak Azhary
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika miaka ya hivi karibuni, suala la kuwawezesha wanawake limekuwa moja ya ajenda muhimu katika jamii ya Misri. Misri imepitia mabadiliko makubwa katika eneo hili, ambapo Baraza la Kitaifa la Wanawake liliandaa Mkakati wa Kitaifa wa kuwawezesha Wanawake 2030. Rais Abdel Fattah El-Sisi aliiagiza serikali na taasisi zote za serikali kufuata mkakati huu kama ajenda ya kazi kwa miaka ijayo na kuhakikisha utekelezaji wa mipango na programu zilizomo. Lengo kuu la mkakati huu ni kuimarisha nafasi ya wanawake katika jamii na kuhakikisha usawa wa kijinsia kwa kuwapa fursa sawa za kielimu, kiuchumi, na kijamii, zitawawezesha kushiriki kikamilifu katika jamii, pamoja na kuwapatia haki zao kama zilivyobainishwa na sheria.
Mkakati huu unaangazia maeneo makuu manne:
1. Kuwawezesha Kisiasa – Kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na kuwakilisha wanawake katika taasisi za kufanya maamuzi.
2. Kuwawezesha Kiuchumi: Kuunga mkono na wanawake katika nyanja za kiuchumi na kutoa fursa ili kuimarisha ushiriki wao katika soko la ajira.
3. Kuwawezesha Kijamii – Kuzingatia suala za ulinzi wa kijamii na kuhakikisha mazingira salama kwa wanawake.
4. Ulinzi – Kulinda haki za wanawake na kupambana na aina zote za ukatili na ubaguzi dhidi yao.
Mkakati huu inaakisi malengo ya kina ya Dira ya Maendeleo ya Misri 2030, na inalingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, hasa lengo la tano linalohusu usawa wa kijinsia.
Ili kufanikisha hilo, Misri imepitisha sheria mbalimbali zinazolenga kulinda haki za wanawake, kama vile sheria dhidi ya ukatili, unyanyasaji wa kijinsia, na ubaguzi. Sheria hizi zinalenga kuunda mazingira ya kisheria yanayohakikisha usawa kati ya wanawake na wanaume. Aidha, kuanzishwa kwa Kituo cha Uangalizi wa Wanawake wa Misri kama chombo huru kunalenga kuhakikisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkakati huo kupitia utekelezaji sahihi na endelevu wa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini.
Serikali ya Misri imezindua mipango mbalimbali inayolenga kuboresha kiwango cha maisha kwa wanawake na kwa jamii kwa ujumla. Mipango hii inajumuisha ufadhili wa miradi midogo na kutoa msaada wa kifedha kwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta mbalimbali. Moja ya mipango hii ni Haya Karima (Maisha Bora), inayolenga kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa kuwahamisha katika mazingira bora na kuboresha miundombinu. Aidha, Mradi wa Maendeleo ya Familia unatekelezwa kwa mtazamo wa maendeleo ya jumla, na mojawapo ya vipengele vyake ni kuzingatia uwezeshaji wa kiuchumi na kifedha kwa wanawake. Kuna pia mipango ya kiafya inayozingatia afya ya wanawake, kama vile Mpango wa Afya ya Mwanamke wa Misri kwa uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti na uchunguzi mwingine wa kitabibu, pamoja na mipango kama Bahya, Ahmi Misr Bahya Fi Dahrak (Linda Misri, Bahya Iko Katika Mgongo Wako) na Sayedat Misr (Wanawake wa Misri).
Misri imechukua hatua mbalimbali kulinda wanawake dhidi ya ukatilii na ubaguzi, ikiwemo kuanzisha kitengo cha kwanza cha kulinda wanawake dhidi ya ukatilii mwaka 2021, na kuboresha mfano wa kitaifa wa ripoti za kesi za ukatilii kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa sera hizo ni makubaliano ya kimaadili ya kuimarisha mazingira salama ya kazi, vitengo vya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia katika vyuo vikuu, na idara za kupambana na ukatilii katika wizara ya mambo ya ndani na haki. Aidha, kamati ya uratibu ilianzishwa ili kumaliza ukeketaji wa wanawake, jambo lililosaidia kupunguza kiwango cha ukeketaji kutoka asilimia 21% mwaka 2014 hadi 14% mwaka 2021. Misri pia imezindua kampeni za mtandao ili kufahimisha watu kuhusu hatari za ukatilii za mtandao, kama vile kampeni ya Takallami (sema) na kampeni ya uwezeshaji wa wanawake ili kujisikia salama kwenye mitandao ya kijamii. Vilevile, ofisi ya malalamiko ya Baraza la Kitaifa la Wanawake inatoa msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa wanawake waliokumbwa na ukatilii. Vilevile, wamewafunza wataalamu waliobobea katika masuala ya wanawake, wakiwemo wahudumu wa afya, maafisa wa polisi, majaji, na wawakilishi wa vitengo vya kupinga ukatili, ili waweze kushughulika vyema na waathirika.
Katika miaka ya hivi karibuni, Misri imefanya juhudi kubwa kuongeza uelewa kuhusu haki za wanawake kupitia kampeni mbalimbali za ufahamu, ikiwa ni pamoja na kampeni za moja kwa moja na zile za mtandaoni, ambapo kampeni hizo zimewafikia wanawake milioni 48. Aidha, kanuni ya kwanza ya vyombo vya habari kuhusu namna ya kuwasilisha masuala ya wanawake imetolewa, na juhudi zimeongezwa kukabiliana na changamoto wakati wa janga la COVID-19 kwa kupitisha sera za haraka za kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na maamuzi 165 ya kuunga mkono wanawake.
Misri pia imeandaa dira ya kimataifa kuhusu wanawake na mazingira, na imezindua mpango wa 'Mwanamke wa Afrika na Ustahimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi'. Katika ngazi ya kimataifa, Misri ilikaribisha makao makuu ya Shirika la Maendeleo ya Wanawake la Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), na ilishinda kiti katika Kamati ya Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW). Vilevile, inafanya kazi ya kufunga pengo la kijinsia kwa kushirikiana na Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum).
Kwa ujumla, juhudi za Misri katika kuwawezesha wanawake zinaonyesha dhamira ya kweli ya kufanikisha usawa wa kijinsia na kuimarisha nafasi ya mwanamke katika nyanja zote za maisha. Kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Kuwezesha Wanawake ifikapo mwaka 2030, ambao unajumuisha maeneo mbalimbali ya kipaumbele, pamoja na sheria, mipango na miradi ya kitaifa, serikali inaonyesha azma yake ya kujenga jamii yenye haki na usawa zaidi. Yale ambayo yamefikiwa hadi sasa ni hatua kubwa kuelekea kuwawezesha wanawake wa Misri, lakini bado kuna haja ya juhudi zaidi na mshikamano kati ya taasisi za serikali na mashirika ya kiraia ili kuhakikisha kuendelea kwa mafanikio haya na kufanikisha mustakabali bora kwa wanawake wote wa Misri.