Mwalimu Nyerere: Baba wa Taifa na Nguzo ya Uhuru wa Tanzania

Imeandikwa na: Bosco Danda
1. Utangulizi:
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa mwanasiasa, mwanafalsafa, na kiongozi wa harakati za ukombozi ameyezaliwa mwaka 1922. Alijulikana kama “Baba wa Taifa” kwa mchango wake mkubwa katika kuipatia Tanganyika (sasa Tanzania) uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza mwaka 1961.
2. Nafasi ya Julius Nyerere katika Uhuru wa Tanzania:
(i) Kiongozi wa kisiasa aliyeelimika:
Nyerere alikuwa miongoni mwa Waafrika wa mwanzo kupata elimu ya juu (Chuo Kikuu cha Edinburgh – Uingereza), jambo lililomsaidia kupambana kwa hoja dhidi ya ukoloni.
(ii) Kuanzisha TANU (1954):
Aliunda Tanganyika African National Union (TANU), chama kilichoongoza mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika kwa njia ya amani.
(iii) Kupigania uhuru kwa njia ya amani:
Tofauti na baadhi ya mataifa ya Afrika, Nyerere aliongoza harakati za kudai uhuru kupitia diplomasia, mazungumzo na siasa safi, bila kutumia vita.
(iv) Kuunganisha Watanganyika:
Kwa ushawishi wake, aliunganisha makabila zaidi ya 120 na kuyafanya kuwa taifa moja lenye mshikamano na lengo la pamoja la kufanikisha uhuru.
(v) Kuwa Waziri Mkuu wa kwanza (1961):
Baada ya uhuru, aliteuliwa Waziri Mkuu wa kwanza, kisha akawa Rais wa kwanza wa Tanganyika mwaka 1962, na Rais wa kwanza wa Tanzania mwaka 1964 baada ya Muungano na Zanzibar.
3. Maadili na Dira ya Uongozi:
(a) Alisisitiza umoja, elimu kwa wote na maendeleo ya watu.
(b) Alianzisha Azimio la Arusha (1967) lililolenga kujenga jamii yenye usawa kupitia ujamaa na kujitegemea.
(c) Alikuwa kiongozi aliyeamini katika maadili, haki na utumishi wa umma.
4. Hitimisho:
Mwalimu Nyerere alikuwa nguzo kuu ya kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika. Aliamini katika usawa, amani na maendeleo ya wote. Ameacha urithi mkubwa wa mshikamano wa kitaifa, amani na heshima ya kimataifa kwa Tanzania.