Siku moja... Balozi wa Italia alimkabidhi Mkuu wa Fasihi ya Kiarabu, Taha Hussein, shahada ya udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Palermo na tafsiri ya Kiitalia ya wasifu wa “Siku”

Siku moja... Balozi wa Italia alimkabidhi Mkuu wa Fasihi ya Kiarabu, Taha Hussein, shahada ya udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Palermo na tafsiri ya Kiitalia ya wasifu wa “Siku”

Imetafsiriwa na: Noran Ahmed Mohammed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Chuo Kikuu cha Palermo, mji mkuu wa Sicily nchini Italia, kilimtunuku Mkuu wa Fasihi ya Kiarabu, Dkt. Taha Hussein, shahada ya udaktari wa heshima mnamo mwaka 1965. Chuo hicho kilimwalika kutembelea Sicily ili kukabidhiwa shahada hiyo katika hafla maalumu, lakini hakuhudhuria kutokana na sababu za kiafya.

Mnamo Machi 21, mwaka 1966, siku kama ya leo, Balozi wa Italia mjini Cairo, Vincenzo Suro, alifika katika villa ya Taha Hussein “Ramtane” huko Haram, na kumkabidhi shahada hiyo. Tukio hilo lilihudhuriwa na Dkt. Abdul Qadir Hatem, Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Suleiman Hazin, Waziri wa Utamaduni, na Bw. Youssef, Waziri wa Elimu, kama lilivyoripotiwa na gazeti la Al-Ahram toleo la Machi 22, 1966.

Al-Ahram linaripoti kwamba Balozi wa Italia alitoa hotuba kuhusu mchango wa Taha Hussein katika fasihi na jinsi wataalamu wa Mashariki wa Italia walivyovutiwa na maandiko yake. Kisha alimkabidhi tafsiri ya Kiitalia ya sehemu ya kwanza ya kitabu chake “Siku” pamoja na neno la kujitolea. Taha Hussein, kwa upande wake, alijibu hotuba hiyo kwa shukrani.

Gazeti hilo linabainisha kwamba shahada ya heshima kutoka Palermo ilikuwa ya saba kwa Taha Hussein, na kwamba pendekezo la kuitunuku lilitolewa na Muitaliano aliyezaliwa Misri, ambaye kwa kipindi fulani alifundisha katika shule ya biashara huko Giza.

Bi. Suzanne, mke wa Taha Hussein, anakumbuka tukio hili katika kumbukumbu zake “Pamoja Nawe” (iliyotafsiriwa na Badr al-Din Ardurki na kuhakikiwa na Mahmoud Amin al-Alam). Anaeleza:
“Balozi wa Italia, Vincenzo Suro, alikuja akiwa ameandamana na ujumbe rasmi, waandishi wa habari na wapiga picha. Alipomkabidhi Taha shahada mpya, alimpa pia zawadi kwa heshima ya kutimiza miaka sabini, kitabu kizuri kuhusu yeye kilichofungwa kwa ngozi nyekundu. Alimpa vilevile nakala ya tafsiri ya Kiitalia ya sehemu ya kwanza na ya pili ya kitabu ‘Siku’, pia iliyofungwa kwa ngozi nyekundu. Balozi alitoa hotuba yenye mvuto, na Taha alimjibu kwa heshima, kisha wakaagana kwa kusita baada ya saa iliyochelewa, kila mmoja akibaki na hisia nzuri kuhusu mwingine.”

Dkt. Muhammad Hassan Al-Zayyat, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri wakati wa Vita vya Oktoba 1973 na mume wa binti ya Taha Hussein, anaeleza katika kitabu chake “Baada ya Siku” baadhi ya mazungumzo yaliyofanyika kati ya balozi na Taha Hussein.

Anaandika kwamba afya ya Taha Hussein ilikuwa dhaifu baada ya upasuaji wa mwaka 1961, jambo lililomfanya ashindwe kusafiri hadi Palermo kupokea shahada hiyo binafsi.
Kuhusu mazungumzo yao, Al-Zayyat anasema:
“Balozi alizungumza kuhusu mji wa Palermo na umaarufu wake katika karne ya kumi na tatu kama mji wa lugha tatu: Kiyunani, Kilatini, na Kiarabu. Alieleza jinsi ulivyorithi ustaarabu mkubwa wa Mediterania: ule wa Wagiriki na ule wa Waarabu.”
Al-Zayyat anaongeza:

“Taha Hussein alimwambia balozi kwamba Waarabu wa kisasa wamezembea katika kuchunguza kipindi hicho cha kihistoria, vivyo hivyo Italia. Alisisitiza umuhimu wa vyuo vikuu kuimarisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sicily, ili pande zote ziweke mkazo zaidi katika kuchunguza enzi za ustaarabu wa Kiarabu na Kiislamu katika nchi na visiwa vya Mediterania. Alisema kwamba Misri imepiga hatua katika mwelekeo huo kupitia kuanzishwa kwa Taasisi ya Madrid nchini Uhispania, na kwamba hatua kama hizo zinastahili kuongezwa na kupanuliwa siku zijazo.”

Kisha mazungumzo yakahamia kwenye kitabu “Siku”, ambacho balozi alibeba tafsiri yake ya Kiitalia. Taha Hussein alisema kuwa hakukumbuka tena idadi kamili ya lugha ambazo kitabu hicho kilishatafsiriwa, iwe barani Ulaya Magharibi, Ulaya Mashariki, Asia, Afrika au Amerika zote.
Balozi akaongeza:
“Nimesikia kwamba kitabu hiki pia kimetolewa kwa maandishi ya Braille kwa vipofu katika lugha kadhaa.”

Taha Hussein akajibu:
“Ndiyo, kimetolewa kwa lugha ya Kiarabu kwa njia hiyo zaidi ya miaka kumi iliyopita, na niliandika utangulizi maalum kwa toleo hilo, nikamkabidhi mwanafunzi wangu, Dkt. Abdul Hamid Younis. Nilisisitiza humo kwamba jambo muhimu maishani ni kuishi kwa tabasamu, kwa bidii, kubeba sehemu ya mizigo yake na kutimiza majukumu yake, huku akiwapenda watu kama anavyojipenda, na kuwatendea wema kama anavyotamani kutendewa. Baada ya hapo, haijalishi iwapo maisha ni mazito au mepesi, na kama watu wanaridhika au la.”

Al-Zayyat anahitimisha kwa kusema kuwa, alipokuwa akiagana na balozi, Taha Hussein alimshukuru kisha akasema:
“Tutakuwa tukisafiri Italia msimu huu wa joto kama ilivyo desturi yetu, na huenda meli ikasimama Sicily safari hii, ingawa mara chache hufanya hivyo, ili niweze kuwashukuru watu wa chuo kikuu binafsi kwa heshima hii kubwa.”