MUSTAKABALI WA ELIMU VIJIJINI

Imeandikwa na: Rogers Richard
Tanzania: Je, hatua zinapigwa na kuna mwanga?
Kumekuwa na changamoto mbalimbali katika utoaji wa elimu Tanzania, hasa katika mazingira ya vijijini.
Changamoto hizo ni kama ifuatavyo:
• Mwamko mdogo wa wazazi kupeleka watoto shule, hasa watoto wenye ulemavu. Wazazi wengi, kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya faida za elimu, wamekuwa wakiwahimiza watoto wao kuolewa badala ya kuendelea na masomo.
• Upungufu wa walimu: Vijijini, walimu wa masomo ya sayansi, hisabati na lugha ni wachache, na wengi hukimbilia mijini kwa sababu ya mazingira bora ya kazi na huduma za kijamii.
• Miundombinu duni: Shule nyingi vijijini bado hazina madarasa ya kutosha, vitabu wala maabara.
• Umbali mrefu: Wanafunzi, hasa wa kike, hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule. Hii imekuwa changamoto katika mahudhurio na kuongeza hatari ya mimba za utotoni au kuacha shule.
HATUA ZINAZOPIGWA NA MWANGA KATIKA KUTOA ELIMU
Pamoja na changamoto hizo, kumekuwa na jitihada kubwa kutoka kwa serikali na mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yameyokuwa mstari wa mbele kutoa misaada ili kuboresha elimu, hasa vijijini. Katika suala la utoaji wa elimu nchini Tanzania, kwa ngazi ya shule za msingi na sekondari, kumekuwa na hatua kubwa sana za serikali kufanikisha lengo la kila Mtanzania kupata elimu.
Katika miaka ya hivi karibuni, imeshuhudiwa utoaji wa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Aidha, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na shule za msingi (darasa la kwanza) pamoja na sekondari (kidato cha kwanza) kupitia sera ya elimu bure. Sera hii ya serikali imewezesha watoto wengi zaidi wa vijijini kujiunga na shule, na hivyo kupunguza mzigo wa wazazi. Zaidi ya wanafunzi 974,332 wamepata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025.
Tanzania imeboresha utoaji wa elimu kupitia ujenzi wa shule nyingi zaidi ili kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi na kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia. Kumekuwa pia na uhamasishaji wa elimu ya wasichana, ambapo programu maalumu zimeanzishwa kuhakikisha wasichana wanabaki shuleni licha ya changamoto za kijamii kama mimba na ndoa za utotoni.
Mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa mstari wa mbele kutoa misaada ya vitabu, madaftari, taulo za kike na hata kujenga madarasa vijijini.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu nchini Tanzania, serikali itaendelea kuongeza bajeti ya elimu, kuimarisha mazingira ya walimu vijijini, na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuongeza ufaulu vijijini na kuondoa tofauti za kielimu kati ya mijini na vijijini.