Balozi Amr El-Gweily… Sauti Thabiti ya Misri katika Medani za Diplomasia ya Kimataifa

Balozi Amr El-Gweily… Sauti Thabiti ya Misri katika Medani za Diplomasia ya Kimataifa

Imetafsiriwa na: Mohamed Hany
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika mazingira ya kimataifa yenye mabadiliko ya haraka na kasi kubwa, jina la Balozi Amr El-Gweily linajitokeza kama nguzo kuu ya diplomasia ya kisasa ya Misri, akichanganya hekima ya kisiasa, mtazamo wa kitaaluma na uwakilishi wa pande nyingi unaoakisi uzito wa nafasi ya Misri katika majukwaa ya kimataifa.

Kwa sasa, El-Gweily anashikilia wadhifa wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayehusika na mambo ya pande nyingi na usalama wa kimataifa. Wadhifa huu unahitaji uwezo wa hali ya juu wa kushughulikia mafaili magumu ya kisiasa, huku akiongeza mchango wa Misri katika masuala ya usalama na amani duniani. Nafasi hii ni kilele cha safari ndefu ya kujitolea na kazi ya kibalozi ya hali ya juu, iliyopitia miji mikuu na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Tangu mwanzo wa kazi yake ya kidiplomasia, El-Gweily ameiwakilisha nchi yake katika vituo muhimu kama Washington, Geneva na New York, ambapo alihusiana moja kwa moja na masuala ya Umoja wa Mataifa na Shirika la Biashara Duniani. Baadaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Misri nchini Serbia (2018–2022), ambako aliongoza awamu mpya ya mahusiano ya pande mbili, kabla ya kuteuliwa mshauri wa kimkakati wa Naibu Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, akitumia juhudi zake kusukuma mbele ajenda za bara katika usalama na maendeleo.

Katika kiwango cha diplomasia ya pande nyingi, El-Gweily aliwahi kuongoza ujumbe wa kitaifa wa Misri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2016, na akaongoza pia mazungumzo nyeti ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Biashara Duniani. Majukumu hayo yalimjumuisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa mwaka 2015, pamoja na kusimamia mazungumzo ya Mkataba wa Teknolojia ya Habari katika WTO mnamo mwaka 2007.

Mchango wake hauishii kwenye siasa pekee, bali pia umeenea katika taaluma na vyombo vya habari. Amewahi kufanya kazi kama mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Amerika mjini Kairo kwa zaidi ya muongo mmoja, ni mjumbe wa jopo la wahariri wa jarida la Siasa za Kimataifa la Shirika la Al-Ahram, na kwa sasa ni mtafiti mwandamizi mgeni katika Taasisi ya Masomo ya Kisiasa na Kistratejia ya Misri.

Kuhusu elimu yake, El-Gweily anashikilia Shahada ya Uzamili katika Mahusiano ya Kimataifa kutoka Shule ya Uchumi ya London, pamoja na Stashahada ya Juu katika Diplomasia ya Kisasa kutoka Chuo Kikuu cha Malta kwa ushirikiano na Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR). Pia ana Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Amerika mjini Kairo na Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Kairo. Hii inamfanya kuwa miongoni mwa wanadiplomasia wachache waliochanganya uelewa wa kisheria na mtazamo wa kisiasa.

Mbali na hayo, El-Gweily anaendeleza ushiriki wake katika maisha ya kiraia na diplomasia ya wananchi, akiwa Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Mabalozi wa Afrika, mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Kusini Duniani cha Sayansi ya Kisiasa, pamoja na mwanachama wa Klabu ya Wanadiplomasia wa Misri na Chama cha Wahitimu wa Uingereza nchini Misri.

Kwa utulivu na kujiamini, Balozi Amr El-Gweily anaendeleza jukumu lake kama balozi wa kipekee wa Misri; mwanadiplomasia mwenye mtazamo wa kimkakati na kiongozi wa kitaifa. Anaamini kwamba jukumu la nchi yake halihusiani tu na kulinda maslahi yake, bali pia linapanuka kuunga mkono masuala ya kibinadamu na haki za kimataifa.