Nuria Sanz Gallego: Mwanakiolojia Anayeongoza Mazungumzo ya Kimataifa kati ya Urithi, Sayansi na Mazingira

Nuria Sanz Gallego: Mwanakiolojia Anayeongoza Mazungumzo ya Kimataifa kati ya Urithi, Sayansi na Mazingira

Imetafsiriwa na: Shahd Gamal
Imehaririwa na: Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr 

Miongoni mwa majina yanayong’aa katika uwanja wa utamaduni wa kimataifa, anang’aa Dkt. Nuria Sanz Gallego, mtaalamu wa Kihispania katika masomo ya akiolojia na anthropolojia, ambaye ameweza kugeuza shauku yake kwa urithi wa binadamu kuwa njia ya kazi yenye ushawishi mkubwa katika ulingo wa kimataifa, ndani ya taasisi kubwa kama UNESCO, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Baraza la Ulaya.

Nuria anamiliki shahada mbili za uzamivu: ya kwanza katika masomo ya kabla ya historia kutoka Chuo Kikuu cha Complutense, Madrid, na ya pili katika masuala ya mazingira ya binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Tübingen, Ujerumani. Hii imemwezesha kuunganisha kina cha kihistoria na uelewa wa kisayansi kuhusu mazingira na uhusiano wa binadamu kupitia nyakati. Tangu mwaka 1995, alijiingiza katika kazi za kimataifa za pande nyingi, akiwa sauti ya kisayansi thabiti na mtetezi jasiri wa urithi wa asili na kitamaduni wa binadamu.

Mnamo mwaka 2009, alipewa jukumu la kuwa mratibu wa kimataifa wa urithi wa sanaa za miamba katika UNESCO, na hapo akawa rejea ya kimataifa katika uwanja huu mgumu unaounganisha maendeleo ya mwanadamu na usemi wa alama tangu mwanzo wa ustaarabu. Baadaye, alisimamia Kitengo cha Amerika ya Kusini na eneo la Karibea katika Kituo cha Urithi wa Dunia, ambapo aliongoza mojawapo ya miradi mikubwa ya kuorodhesha maeneo katika Orodha ya Urithi wa Dunia: “Mtandao wa Njia za Inca – Qhapaq Ñan”, mradi wenye tamaa kubwa ulioshirikisha nchi sita za Andes na kuweka msingi wa mtandao mkubwa zaidi wa maarifa ya anthropolojia katika eneo hilo.

Mnamo mwaka 2013, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi na Mwakilishi wa UNESCO nchini Mexico, ambapo alisimamia zaidi ya miradi thelathini iliyohusu maarifa ya jadi, urithi hai wa kitamaduni-jamii wa jamii za vijijini, viwanda vya ufundi, na utofauti wa lugha, pamoja na programu ya kisayansi kuhusu chimbuko la uzalishaji wa chakula na maendeleo endelevu. Hatua hizi hazikuwa miradi ya kawaida pekee, bali zilikuwa ramani ya maendeleo yanayozingatia heshima kwa urithi hai.

Nuria pia anajulikana kwa jukumu lake la kuanzisha mpango wa kimataifa wa UNESCO kuhusu mtaji wa kisayansi na kibinadamu kwa ajili ya maendeleo ya mwanadamu (HEADS), uliokutanisha zaidi ya wanasayansi 250 kutoka taaluma mbalimbali — kuanzia paleontolojia, anthropolojia, mazingira, hadi isimu na jiografia ya kibayolojia — ili kuunda mtandao wa maarifa ya fani mchanganyiko ambao bado unaendelea hadi leo. Amehariri juzuu saba za kielimu katika muktadha huu ambazo zinachukuliwa kama rejea muhimu ya kimataifa.

Mbali na kazi zake za kisayansi, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Kikundi cha Sanaa cha UNESCO, ambapo aliweka mpango kazi wenye tamaa kubwa kwa kikundi hicho, na kusimamia kuchapishwa kwa katalogi mbili za sanaa, pamoja na kitabu kilichotolewa mahsusi kwa ajili ya sanaa ya Kiafrika, jambo linalodhihirisha mtazamo wake wa kuunganisha sayansi na sanaa.

Leo hii, kwa mwaliko wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), anashikilia nafasi ya mshauri mkuu katika Kitengo cha Uanuwai wa Kibiolojia na Mabadiliko ya Tabianchi, ambapo anaongoza mpango wa kazi wa pamoja kati ya UNESCO na FAO. Katika kazi yake ya sasa, anazingatia historia ya mabadiliko ya chakula tangu enzi za kabla ya historia, umuhimu wa maarifa ya jadi katika uzalishaji na ulaji wa chakula, na jinsi urithi huu wa kibinadamu unavyoweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Hakika, wasifu wa Dkt. Nuria Sanz Gallego siyo tu safari ya kielimu au kitaaluma, bali ni simulizi ya mwanamke aliyejitolea maisha yake kukusanya nyuzi za zamani ili kuelewa wakati wa sasa na kujenga mustakabali ulio na utu zaidi, utofauti na maendeleo endelevu.