Mostafa Magdy… Kijana wa Misri anayebobea katika kuunganisha upangaji na utekelezaji katika kuhudumia masuala ya vijana na maendeleo
Imetafsiriwa na: Mahmoud Mohamed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Mustafa Magdy ni mojawapo wa vijana mashuhuri wa Misri waliothibitisha uwepo wao wenye nguvu katika masuala ya sera za umma, maendeleo ya vijana, na kazi ya kitaasisi ndani na nje ya nchi. Tangu kujiunga kwake mapema na huduma za kijamii, amekuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wa Kimasri, akionesha uwezo wa kusawazisha kati ya maono ya kimkakati na utekelezaji wa vitendo, akitegemea msingi thabiti wa kielimu na tajiriba kubwa ya uwanjani.
Kwa sasa, Magdy anashikilia wadhifa wa Msaidizi wa Waziri wa Vijana na Michezo kwa Masuala ya Kistratejia na Taarifa tangu Septemba 2024. Vilevile, anaongoza Kitengo cha Uundaji wa Sera na Uchanganuzi wa Biashara katika ofisi ya Waziri. Aidha, ni mwanachama hai wa Uratibu wa Vijana wa Vyama na Wanasiasa, pamoja na Sekretarieti ya Ufundi ya Baraza la Vijana la Kimataifa la Pande Mbili. Nafasi hizi zimemuweka katika mstari wa mbele kama mdau muhimu katika uundaji wa maamuzi ya vijana nchini Misri.
Magdy ameshiriki kwa bidii katika maandalizi ya mashindano makubwa ya michezo yaliyofanyika Misri, ambapo alihudumu kama Katibu Mkuu wa Kamati ya Kudumu ya Usimamizi wa Wajitoleaji katika matukio makubwa ya michezo. Alisaidia pia katika maandalizi ya vijana kwa ajili ya mashindano kama Kombe la Dunia la Mpira wa Mkono na Kombe la Mataifa ya Afrika.
Aidha, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Jukwaa la Kitaifa la Vijana, na akawa kiunganishi cha Wizara ya Vijana na Michezo katika jukwaa la Shabab Balad linaloendeshwa na Wizara ya Ushirikiano wa Kimataifa kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa. Jukumu hili limeonesha uaminifu wake kitaasisi na kuimarisha nafasi yake katika medani ya kimataifa.
Shughuli zake pia zinaenea kwenye uwanja wa kitaaluma, ambapo anafanya kazi kama Msaidizi wa Mwalimu katika Chuo cha Usimamizi, Teknolojia, Kompyuta na Teknolojia ya Habari cha Chuo cha Kiarabu cha Sayansi, Teknolojia na Usafirishaji Baharini. Aidha, ni mjumbe wa bodi ya Shirikisho la Kimasri la Michezo ya Kielektroniki, na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Ushirikiano wa Kimataifa katika shirikisho hilo. Vilevile, ni mratibu wa Bodi ya Wadhamini wa Mji wa Michezo katika mji mkuu mpya wa kiutawala, na mratibu mkuu wa maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa wa Vijana na Watoto wa Misri.
Kabla ya hapo, Magdy alifanya kazi kama mpangaji mkakati katika Baraza la Kitaifa la Ushindani la Misri, ambapo alihusika kuchambua viashiria vya ushindani wa kimataifa, na alikuwa mjumbe wa kamati ya uratibu ya Jukwaa la Misri la Kuunga Mkono Ajira ya Vijana, kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani. Pia alishiriki katika mradi wa kuboresha usimamizi wa fedha za umma na ugatuzi wa kifedha, na alichangia kuandaa mikakati ya wizara kadhaa za Misri kama vile Elimu, Utamaduni na Mipango.
Safari yake ya awali ilijulikana kwa shughuli nyingi za kielimu na kijamii; aliongoza Shirikisho la Wanafunzi wa Shule za Kairo, Baraza la Wanafunzi wa Chuo cha Kiarabu cha Sayansi na Teknolojia, na alikuwa mwanachama wa ofisi kuu ya Shirikisho la Wanafunzi wa Jamhuri. Aidha, alishiriki katika mpango wa mazungumzo ya dini na uongozi katika Chuo Kikuu cha Cambridge chini ya Jukwaa la Vijana Watengenezaji Amani kati ya Al-Azhar na Askofu wa Canterbury. Pia aliwakilisha Misri katika Mkutano wa Dunia wa Serikali huko Dubai mnamo mwaka 2019, na Mkutano wa Kiarabu huko Tunisia mnamo mwaka 2020.
Amehitimu katika Programu ya Usimamizi wa Uendeshaji na Miradi kutoka Chuo Kikuu cha Lancashire nchini Uingereza, na pia ni mhitimu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa katika Chuo cha Kijeshi cha Nasser.
Kwa wingi wa nafasi na uzoefu huu, Mustafa Magdy anawakilisha mfano wa kiongozi kijana aliyeweza kuunganisha kati ya fikra za kimkakati na utekelezaji wa kivitendo, kati ya uzalendo na uwazi wa kimataifa, na kati ya kazi za kitaasisi na shughuli za kijitolea, akawa miongoni mwa sauti kuu zenye matumaini makubwa katika mustakabali wa usimamizi na sera za umma nchini Misri.