Makumbusho ya Jeshi la Anga la Misri... Taswira ya Fahari ya Tai wa Anga
Imetafsiriwa na: Yasmin Ibrahim Mohamed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katikati ya Uwanja wa Ndege wa Almaza, mashariki mwa Kairo, lipo moja ya makumbusho ya kijeshi ya kuvutia zaidi nchini Misri: Makumbusho ya Jeshi la Anga la Misri, yaliyozinduliwa tarehe Mei 31, 2016 katika kipindi cha kwanza cha urais wa Abdel Fattah El-Sisi. Makumbusho haya si jengo la kumbukumbu pekee; ni dirisha linaloonesha historia ya utukufu na mashujaa wa anga walioandika hadithi zao kwa ujasiri juu ya anga la taifa.
Wageni wanapoingia katika ukumbi mkuu, wanakutana kwanza na Ukumbi wa Mashahidi, unaohifadhi majina na picha za mashujaa waliotoa maisha yao kwa ajili ya kulilinda taifa. Baadaye, Ukumbi wa Asili ya Kihistoria unawapeleka katika safari ya nyuma hadi mwaka 1928, wakati Bunge la Misri lilipoidhinisha kuundwa kwa kikosi cha anga cha taifa. Safari hii ilianza na maafisa watatu tu Fouad Haggag, Abdel Moneim al-Mikati na Ahmed Abdel Razek waliopata mafunzo nchini Uingereza kabla ya kuruka na ndege zao katika anga la Cairo, wakitangaza kuzaliwa rasmi kwa Jeshi la Anga la Misri.
Maonesho yanabainisha hatua mbalimbali za uanzishwaji na ukuaji wa jeshi hilo, kuanzia kuunganishwa kwake na jeshi la ardhini hadi kutangazwa rasmi mnamo mwaka 1937 kama “Royal Egyptian Air Force” kwa amri ya Mfalme Farouk, baada ya mikataba na makampuni ya Uingereza kuimarisha uwezo wake.
Aidha, makumbusho yanaonesha ushiriki wa Jeshi la Anga katika Vita vya Palestina vya mwaka 1948, na hata tukio maarufu ambapo ndege za Misri zilishambulia kimakosa kambi ya Waingereza huko Ramat David, zikidhani kuwa ni ya Israeli. Nyaraka na vielelezo pia zinaeleza hatua ya baada ya Vita vya Pili vya Dunia, pale Misri ilipoanza kutumia ndege za kisasa zaidi, na wakati huo ndipo rubani wa kwanza wa Misri aliporuka ndege ya jeti.
Baada ya Mapinduzi ya Julai 1952, kikosi kilibadilishwa jina na kuwa Jeshi la Anga la Misri, na kuingia katika enzi mpya ya kisasa, hasa kwa msaada wa ndege za Kisovieti kama MiG-15 na Yak-11 zilizotumika sana katika vita vya baadaye. Makumbusho haya pia yanaelezea miaka migumu ya kushindwa, hasa katika vita vya Juni 1967, ambapo ndege nyingi za Misri ziliharibiwa ardhini kabla ya kupaa. Hata hivyo, rubani shujaa Mohamed Abbas Helmy aliandika ukurasa wa kipekee wa ujasiri kwa kurusha ndege ya mafunzo na kuishambulia kambi ya Israeli, akitoa ishara ya ujasiri na matumaini licha ya hali ngumu.
Kisha ikafuata Vita vya Uvumilivu, ambavyo vilijenga upya roho ya jeshi chini ya uongozi wa Luteni Jenerali Madkour Abu El-Ezz. Yeye alisimamia ukarabati na urejeshaji wa zaidi ya ndege 250, akiandaa Jeshi la Anga kwa ajili ya vita vipya vya heshima.
Shambulio la anga la tarehe Oktoba 6, 1973 liliashiria mwanzo wa safari ya ushindi. Ndege za Misri zilivuka Mfereji wa Suez na kusaidia kurejesha ardhi ya Sinai, iliyokuwa ikikaliwa kwa miaka sita.
Kutembea ndani ya Makumbusho ya Jeshi la Anga la Misri si kutazama ndege na vielelezo pekee; ni kusimama ana kwa ana na historia ya taifa, historia iliyoandikwa angani na marubani wake, ikitiwa sahihi kwa damu ya mashahidi na ndoto ya Misri ya kumiliki na kulinda anga yake milele.