Boutros Boutros Ghali... Mwarabu na Mwafrika wa kwanza ashika cheo cha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
"Ujenzi wa Amani ni suala linalohusu mataifa yote. Vita na demokrasia, vita na maendeleo haviendani pamoja, kwa maana nyingine amani itakuwa sharti muhimu la kuhakikisha demokrasia na kueneza utamaduni wa amani na maarifa katika maana yake kamili."
Yeye ni mmoja wa wanadiplomasia wa Misri, anayechukuliwa kama mtaalamu wa sheria za kimataifa, mwanasayansi na mwandishi ambaye maandishi yake yalichapishwa sana, pia alishika cheo cha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Boutros Boutros Ghali alizaliwa tarehe 14, mwezi wa Novemba, mwaka wa 1922, mjini Kairo, naye ni mjukuu wa Boutros Nayrouz Ghali, Waziri Mkuu wa Misri mwanzoni mwa karne ya 20. Mnamo wa mwaka wa 1946, Ghali alihitimu kutoka Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Kairo, na mnamo wa mwaka wa 1947, alipata diploma ya sayansi ya siasa, uchumi, na sheria ya umma kutoka Chuo Kikuu cha Paris, kisha akapata Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Sorbonne mnamo wa mwaka wa 1949, na tasnifu yake ilikuwa kuhusu utafiti wa mashirika ya kikanda.
Aliporudi Kairo, alifanya kazi kama profesa na mkuu wa Idara ya Sheria ya Kimataifa na Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kairo katika kipindi cha (1949-1977). Na wakati wa kipindi hicho, Dkt. Boutros Ghali alikuwa mwanasayansi na mtafiti kwa Udhamini wa Fulbright katika Chuo Kikuu cha Columbia (1954-1955), na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti katika Chuo cha Lahai la Sheria ya Kimataifa (1963-1964); na profesa mgeni katika Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Paris (1967-1968). Na amefundisha kuhusu sheria za kimataifa na mahusiano ya kimataifa katika vyuo vikuu Barani Afrika, Asia, Ulaya, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini.
Dkt. Boutros Ghali alianzisha jarida la "Al-Ahram ya kiuchumi" kuanzia kipindi cha 1960-1975 na alikuwa mhariri wake, pamoja na jarida la robo mwaka la Al-Siyasa Al-Dawlaiya, ambalo alihariri hadi mwezi wa Desemba, mwaka wa 1991. Machapisho na makala nyingi -zaidi ya 100 zilizoandikwa na Dkt. Boutros Boutros Ghali- zinahusika na masuala ya kikanda na kimataifa, sheria na diplomasia, na sayansi ya kisiasa. Pia alishika cheo cha mwenyekiti wa Jumuiya ya Misri ya Sheria za Kimataifa tangu mwaka wa 1965, na uanachama wa Kamati Kuu na Ofisi ya Kisiasa ya Muungano wa Ujamaa wa Kiarabu katika kipindi cha 1974-1977.
Alishika Cheo cha mwenyekiti wa Kituo cha Mafunzo ya Kisiasa na Kimkakati (Al-Ahram) tangu mwaka wa 1975, mjumbe wa Bodi ya Utawala ya Wadhamini ya Chuo cha Sheria ya Kimataifa cha Lahai tangu mwaka wa 1978, mjumbe wa Kamati ya Kisayansi ya Chuo cha Amani cha Dunia (Monton, Ufaransa), mwanachama mshiriki wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa (Roma) tangu mwaka wa 1979, na alikuwa mjumbe wa Kamati ya Matumizi ya Mikataba na Mapendekezo ya Shirika la Kazi Duniani kutoka mwaka wa 1971 hadi 1979.
Alikuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chama cha Kitaifa cha Demokrasia mnamo wa mwaka wa 1980, na mnamo 1987 akawa mjumbe wa Bunge la Misri. Ghali alishika cheo cha Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje kuanzia Oktoba (1977-1991).
Dkt. Boutros Boutros Ghali alihudhuria mkutano wa kilele huko Camp David na alikuwa na jukumu katika mazungumzo yanayohusiana na Makubaliano ya Camp David kati ya Misri na Israeli, yaliyotiwa saini mnamo wa mwaka wa 1979. Na aliongoza wajumbe kadhaa wa Misri kwenye mikutano ya Umoja wa Nchi Huru ya Afrika, Harakati ya Nchi Zisizofungamana kwa upande wowote, vilevile Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Ufaransa, pamoja na kuuongoza ujumbe wa Misri kwenye vikao vya Jumuiya kuu mnamo miaka ya 1979, 1982 na 1990.
Pia alishika cheo cha Naibu Waziri Mkuu wa Mambo ya Nje wa Misri tangu Mei, mwaka wa 1991, hadi Jumuiya Kuu ya Umoja wa Mataifa ilipomteua tarehe 3, mwezi wa Desemba, mwaka wa 1991, ambapo alikuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa, ambapo alianza majukumu yake mwezi wa Januari, mwaka wa 1992 kwa kipindi cha miaka mitano.
Alitunukiwa Uzamivu katika Sheria kutoka Taasisi ya Jimbo na Sheria ya Chuo cha Sayansi cha Urusi huko Moscow, mnamo Septemba,1992.
Aliongoza Kamati ya Demokrasia na Maendeleo ya UNESCO mwaka wa 1997, na cheo cha Katibu Mkuu wa Shirika la Francophone kutoka mwaka wa 1998 hadi mwaka wa 2004, na aliongoza Kituo cha Kusini huko Geneva.
Pia alichangia katika kuanzishwa kwa Baraza la Kitaifa la Haki za Kibinadamu nchini Misri na kuliongoza kuanzia mwaka wa 2004 hadi mwaka wa 2011.
Mnamo wa mwezi wa Aprili, mwaka wa 2013, alichaguliwa kama mwenyekiti wa Jukwaa la Kimataifa la meza ya pande zote.
Wakati wa maisha yake ya kazi, Dkt. Boutros Boutros Ghali alipokea tuzo na medali kutoka nchi 24, pamoja na Misri kuna Ubelgiji, Italia, Colombia, Guatemala, Ufaransa, Ecuador, Argentina, Nepal, Luxembourg, Ureno, Niger, Mali, Meksiko, Ugiriki, Chile, Brunei Darussalam, Ujerumani, Peru, Côte d'Ivoire, Denmark, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uswidi na Jamhuri ya Korea . Pia alitunukiwa Medali ya Wapiganaji wa Malta.
Alitunukiwa tuzo kadhaa na digrii za Uzamivu wa heshima, zikiwemo:
Shahada ya Udaktari wa heshima kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Siasa huko Paris, mwezi wa Januari, mwaka wa 1992.
Tuzo ya kumbukumbu ya Christian A. Herter, iliyotolewa na Baraza la Masuala ya Dunia, Boston, mwezi wa Machi, mwaka wa 1993.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Leuven, Ubelgiji, mwezi wa Aprili, mwaka wa 1993.
Tuzo ya "Mtu wa Amani" iliyotolewa na Taasisi ya "Waungaji mkono kwa ajili ya Amani", ambao makao makuu yake ni Italia, mwezi wa Julai, mwaka wa 1993.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Laval, Quebec, mwezi wa Agosti, mwaka wa 1993.
Tuzo ya Arthur A. Houghton, inayojulikana kama tuzo ya "Star Crystal Excellence" iliyotolewa na Taasisi ya Kiafrika ya Marekani, New York, mwezi wa Novemba, mwaka wa 1993.
Uanachama wa Heshima wa Chuo cha Sayansi ya Asili cha Urusi, mwezi wa Aprili, mwaka wa 1994.
Uanachama wa Heshima wa Kigeni wa Chuo cha Sayansi cha Urusi, Moscow, mwezi wa Aprili, mwaka wa 1994.
Uanachama wa heshima wa kigeni katika Chuo cha Sayansi cha Belarusi, Minsk, mwezi wa Aprili, mwaka wa 1994.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Carlos III, Madrid, mwezi wa Aprili, mwaka wa 1994.
Shahada ya heshima kutoka Chuo cha Huduma za Kigeni, Chuo Kikuu cha Georgetown, Mji mkuu wa Washington, mwezi wa Mei, mwaka wa 1994.
Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Moncton, New Brunswick, Canada, mwezi wa Agosti, mwaka wa 1994.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Bucharest, mwezi wa Oktoba, mwaka wa 1994.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Baku, mwezi wa Oktoba, mwaka wa 1994.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Yerevan, mwezi wa Novemba, mwaka wa 1994.
Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha Haifa, mwezi wa Februari, mwaka wa 1995.
Alifariki Dunia Jumanne, tarehe ya 16, mwezi wa Februari, mwaka wa 2013, akiwa na umri wa miaka 93, katika Hospitali ya Kairo baada ya muda mrefu wa maradhi, na mazishi ya kijeshi yalifanyika kwa ajili yake kwa sala iliyoongozwa na Papa wa Kikopitiki Tawadros wa Pili. Alizikwa katika Kanisa la Petro huko Abbasiya, Kairo.