Baraza la Mawaziri la Misri: Akili ya Utekelezaji ya Taifa
Imetafsiriwa na: Sara Mohammed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Baraza la Mawaziri la Misri ndilo chombo kikuu cha utekelezaji katika Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, likijumuisha Waziri Mkuu na mawaziri husika, na linawajibika kusimamia masuala ya dola ndani ya mfumo mkuu wa serikali.
Waziri Mkuu anasimama mbele katika uongozi wa utekelezaji kupitia mamlaka yake ya kutoa kanuni na maamuzi yanayohitajika ili kuwezesha utekelezaji wa sheria, kwa sharti kwamba kanuni hizo hazihusishi marekebisho, kusitisha au msamaha wa kutotumia sheria. Aidha, anaweza kumruhusu mtu mwingine kutoa kanuni hizo, isipokuwa pale ambapo sheria inabainisha chombo maalumu.
Wajibu wa Waziri Mkuu pia unahusisha kufanya maamuzi ya kuanzisha na kuendesha taasisi za umma baada ya kupata idhini ya Baraza la Mawaziri, pamoja na kutoa kanuni za udhibiti zinazohitajika ili kudumisha utulivu wa umma.
Mawaziri, kwa upande wao, wanaongoza wizara mbalimbali kwa kuweka sera za jumla kwa kushirikiana na taasisi husika, na kusimamia utekelezaji wake moja kwa moja, ikiwemo kutoa mwongozo na uangalizi ili kuhakikisha malengo ya taifa yanatimia. Kila wizara hupewa Katibu Mkuu wa kudumu, lengo likiwa kuimarisha uthabiti wa kiutawala na kuongeza ufanisi wa taasisi.
Mamlaka ya serikali yanaenea kwa kushirikiana kikamilifu na Rais wa Jamhuri katika kutengeneza sera kuu za taifa na kufuatilia utekelezaji wake, kuhakikisha usalama wa nchi, kulinda haki za wananchi, pamoja na uratibu kati ya wizara na mashirika ya umma. Pia, serikali inawajibika kuandaa miradi ya sheria na maamuzi na kufuatilia utekelezaji wake kiutawala kwa mujibu wa sheria.
Aidha, inaunda mipango ya maendeleo ya jumla na bajeti kuu ya taifa, na kujadiliana kuhusu mikopo na misaada kulingana na katiba, katika mfumo ulio kamili wenye lengo la kufanikisha ukuaji, utulivu na kutimiza matarajio ya wananchi wa Misri.