Hassan Shehata .. Mwalimu wa Mpira wa Miguu wa Misri

Imefasiriwa na / Ali Mahmoud
Hassan Shehata alizaliwa mnamo Juni 19, 1947, katika Mji wa Kafr Al-Dawwar, Mkoa wa Al-Beheira. Shehata alikua katika familia ya michezo, na akaanza kufanya mazoezi ya Mpira wa Miguu tangu akiwa na umri wa miaka kumi alipokuwa mwanafunzi katika shule ya msingi huko Kafr Al-Dawwar, kisha katika Shule ya Sekondari ya Biashara ya Salah Salem, na kisha akajiunga na Klabu ya Kafr Al-Dawwar, moja ya vilabu vya daraja la pili wakati huo.
Baada ya mechi yake ya majaribio na Timu ya Taifa ya Bahri dhidi ya Timu ya Taifa, Mohamed Hassan Helmy, Mkurugenzi wa timu ya taifa, alimtolea kujiunga na Zamalek, na mnamo Novemba mwaka wa 1966, Shehata alikuwa na umri wa miaka kumi na tisa na katika mechi yake ya kwanza na klabu ya Zamalek alifunga mabao matatu ili Zamalek ishinde kwa mabao manne.
Baada ya kuzuka kwa Vita vya Juni Mwaka wa 1967, mashindano ya ndani nchini Misri yalisimama, kwa hivyo Shehata alijiunga na Klabu ya Kuwaiti Kazma, na akafanikiwa mafanikio kadhaa huko Kuwait, ikiwa ni pamoja na kushinda taji la mchezaji bora katika Bara la Asia, na kwa hivyo Shehata ndiye Mchezaji wa Pekee aliyepokea taji la mchezaji bora katika bara lingine lisipokuwa bara lake la asili, pia alisajiliwa na Jeshi la Kuwait, alishiriki na Timu ya Taifa ya Kuwait katika Mashindano ya kijeshi ya Dunia huko Bangkok nchini Thailand, na pia alishiriki na Timu ya Taifa ya Kuwait katika Mashindano ya Asia.
Mnamo Oktoba mwaka wa 1973, Shehata alirudi Misri kukamilisha kazi yake na Zamalek, na alicheza mechi moja katika tarehe tano ya mwezi huo huo, lakini Vita vya Mwaka wa 1973 vilisimamisha shughuli za Soka za Misri tena.
Shehata alikaa na timu ya Zamalek miaka kumi kamili, ambapo aliteka mioyo ya mashabiki waliomwita “Mwalimu”, na alishinda Ligi ya Misri mara moja katika msimu wa 1977-1978, Kombe la Misri mara tatu, katika misimu ya 1974-1975 na 1976-1977 na 1978-1979. Alifanikiwa kufunga mabao 77 katika Ligi ya Misri, mabao matano katika Kombe la Misri, na mabao sita kwa timu ya Zamalek katika Mashindano ya Afrika.
Hassan Shehata alikuwa maarufu kwa bao alilofunga katika moja ya mechi za Zamalek na Al-Ahly, ambalo lilifutwa kuwa bao la kushangaza zaidi lililofutwa kwa mchezaji kwa sababu ya kupenya. Mashabiki wa Zamalek walizoea kuimba “Hassan Shehata, mwalimu, acha wavu iongee” wakati wowote alipofunga bao.
Katika ngazi ya kimataifa, Shehata alijiunga na timu ya Taifa ya Misri mnamo mwaka wa 1969, ambapo mechi yake ya kimataifa ya kwanza ilikuwa mechi ya kirafiki dhidi ya Timu ya Taifa ya Libya, ambayo Misri ilishinda kwa bao safi lililofungwa na Hanafi Halil na lilifanywa na Shehata. Idadi ya mechi za Hassan Shehata na Timu ya Taifa ya Misri ilifikia jumla ya mechi 70 za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Michuano 4 ya Afrika.
Baada ya kazi hii ndefu ndani ya viwanja, mwalimu Hassan Shehata alishinda taji la mchezaji bora katika Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika katika Mwaka wa 1974, na alikuwa miongoni mwa walioteuliwa kwa Tuzo ya “France Football” kwa Bora Barani Afrika katika Mwaka wa 1974. Pia alipokea tuzo ya “Mchezaji Bora nchini Misri” katika Mwaka wa 1976, na “Medali ya Michezo ya Daraja la Kwanza” katika Mwaka wa 1980.
Na mnamo 1983, Shehata aliamua kustaafu kutoka kucheza mpira wa miguu, na akageuka kuwa kocha, na mwanzo ulikuwa na vijana wa klabu ya Zamalek walio chini ya umri wa miaka 19, wakati ambao alishinda Ubingwa wa Jamhuri kwa vijana mnamo Mwaka wa 1984 na 1985. Katika Mwaka wa 1986, alichaguliwa kama kocha msaidizi wa timu ya Kwanza ya Zamalek, ambayo ilifundishwa na Ninkovic na ilitengwa kwa sababu ya matokeo mabaya, kwa hivyo alisafiri kwenda Emirates kufundisha klabu ya Al Wasl ya Umoja wa Falme za Kiarabu katika Mwaka wa 1986, kisha El-Marrikh ya Misri na Polisi wa Oman, na kisha akarudi kufundisha Klabu ya Al Ittihad ya Alexandria kwa msimu wa 1991-1992.
Wakati wa kazi yake kama kocha, alifanikiwa kuongoza vilabu vitatu vya Misri, navyo ni El-Minya, Al-Sharqiya na Timu ya Taifa ya Suez kupanda kutoka ngazi ya chini kwa Ligi kuu, mnamo kipindi kati ya 1996 na 2000.
Katikati ya Mwaka wa 2000, alipewa jukumu la kufundisha Timu ya Taifa ya Misri chini ya umri wa miaka 16, kisha timu ya Vijana ya Misri, ambayo iliweza kushinda Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika huko Burkina Faso mnamo Mwaka wa 2003, na kupitia kwake Timu ya Taifa ya Vijana, ikiongozwa na Mwalimu, ilihitimu Kombe la Dunia la Vijana. Timu ya Taifa ilifanya Vizuri katika Kombe la Dunia, kwani ilifanikiwa kuendelea hadi raundi ya kumi na sita baada ya kushika nafasi ya tatu katika kikundi chao. Timu hiyo ilikuwa imepata ushindi wa ajabu katika raundi ya kwanza dhidi ya mwenzake wa Uingereza na bao safi lililopigwa na mchezaji Emad Moteab. Na katika raundi ya kumi na sita, timu ilipata hasara mikononi mwa mwenzake wa Argentina katika muda wa ziada baada ya sare kwa matokeo ya 1-1 katika wakati wa awali wa mechi. Kwa hiyo, pazia liliangukia juu ya ushiriki wa timu ya kitaifa katika michuano.
Baada ya kuondoka kwenye Kombe la Dunia la Vijana, Hassan Shehata aliongoza Klabu ya Al Mokawloon Al Arab, ambayo bado ilikuwa ikicheza katika Ligi ya daraja la pili, kushinda Kombe la Misri mnamo Mwaka wa 2004 baada ya kushinda Klabu ya Al-Ahly kwa matokeo ya 2-1, kwa hivyo Al Mokawloon ikawa timu ya kwanza kucheza katika daraja la pili na kushinda ubingwa huu. Kisha Shehata aliongoza Al Mokawloon kushinda Kombe la Super la Misri la mwaka huo huo kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya kuishinda Zamalek, bingwa wa ligi wakati huo kwa matokeo ya 2-4.
Mnamo Oktoba 12, Mwaka wa 2004, Shirikisho la Misri lilimfukuza Marco Tardelli, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Misri, baada ya nafasi ya timu ya taifa katika mechi za kufikia Afrika kwa Kombe la Dunia kuwa ngumu na ukosefu wa matumaini yake ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la Ujerumani. Mnamo tarehe ya Ishirini na nane ya mwezi huo huo (Oktoba 28, 2004) Essam Abdel Moneim, Rais wa Shirikisho la Misri, alitangaza uteuzi wa Shehata kama mkurugenzi wa muda wa kiufundi wa timu ya taifa kuchukua nafasi ya Tradelli.
Kisha mkataba wa muda uligeuka kuwa mkataba wa mwisho mnamo Januari 13, Mwaka wa 2005, baada ya kuacha mkataba na Mjerumani, Theo Boker. Wafanyakazi wa Shehata walijumuisha Shawqi Gharib kama Kocha Mkuu, Hamada Sidqi kama Msaidizi wa Kocha, Ahmed Suleiman kama Kocha wa golikipa na Samir Adly kama Mkurugenzi wa utawala wa Timu.
Timu ya Taifa ya Misri ilipata ushindi kadhaa na matokeo mazuri wa kirafiki mapema na wafanyikazi wake wapya wa kiufundi wakiongozwa na Shehata, ambayo ilirudisha imani ya mashabiki katika timu yao. Timu ya Taifa ya Misri ilianza na sare nzuri kwa bao kwa bao dhidi ya Timu ya Taifa ya Bulgaria jijini Kairo katika mechi ya kwanza ya Timu ya Taifa na uongozi wa Shehata. Kisha, Timu hiyo iliipiga mwenzake wa Korea Kusini kwa bao safi huko Seoul kabla ya kuishinda Timu ya Taifa ya Ubelgiji kwa mabao manne safi jijini Kairo.
Kwa upande wa mechi za kufikia Kombe la Dunia 2006, timu ya taifa ilimaliza mechi zake zilizobaki kwa kufikia pointi 10 kati ya pointi 15. Timu ya Taifa ilikuwa imepata mshangao kwa kutoka sare na mwenzake wa Cameroon na bao kwa bao katika raundi ya mwisho ya kufikia, ili kadi ya kufikia kutoka Cameroon iende kwa timu ya Taifa ya Ivory Coast.
Hassan Shehata aliongoza Timu ya Taifa ya Misri kufikia mara tatu ya kihistoria, kwa kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika mara 3 mfululizo miaka ya 2006 na 2008 na 2010 katika Misri, Ghana na Angola. Pia alifanikiwa katika mashindano ya Michezo ya Kiarabu mnamo Mwaka wa 2007 na kama matokeo ya kutawazwa kwake Afrika, Timu ya Taifa ya Misri Iliruka hadi nafasi ya kumi katika orodha ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kwa Mwezi wa Februari, Mwaka wa 2010 ambayo ni nafasi bora iliyopatikana na Timu ya Taifa ya Afrika katika historia baada ya Timu ya Dhahabu ya Nigeria kuchukua Nafasi ya Tano huko katika Mwaka wa 1994 kisha Timu ya Taifa ya Misri iliendelea hadi nafasi ya tisa katika ukadiriaji wa mwezi wa Julai, Mwaka wa 2010 katika mafanikio ambayo hayakufikiwa na kocha yeyote wa kiufundi ambaye alichukua mafunzo ya mafarao. Kwa hivyo, yeye ndiye mkurugenzi wa wa pekee wa kiufundi ambaye amepata taji la Mataifa ya Afrika na Timu ya Taifa ya Vijana na ya watu wazima ya Misri.
Mnamo Juni 6, Mwaka wa 2011, Samir Zaher, Mkuu wa Shirikisho la Soka la Misri, alitangaza kusitishwa kwa mkataba wa Hassan Shehata na wafanyikazi wake wa kiufundi kutoka kufundisha Timu ya Taifa ya Misri kwa njia ya kirafiki, baada ya Matumaini ya Misri ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 kupungua kabisa. Hivyo pazia juu ya maandamano ya Hassan Shehata na Timu ya Taifa ya Misri liliangukia, ambapo alicheza mechi 96, Timu ya Taifa ilishinda katika mechi 61, sare katika mechi 17 na kupoteza katika mechi 18 na ikifunga mabao 190 na ikifungwa mabao 81 na kutegemea wachezaji 100 aliyeshiriki zaidi ni mlinzi anayeitwa mwamba wa Mwamba Wael Gomaa.
Baadaye, Hassan Shehata alichukua kazi ya meneja wa Timu ya Kwanza ya Soka ya Klabu ya Zamalek mnamo Julai 12, 2011 akimrithi meneja Hossam Hassan, na mkataba ulitangazwa siku iliyofuata.
Jumanne, Oktoba 9, Hassan Shehata alitia saini ya mkataba wa kufundisha Klabu ya Kiarabu ya Qatar, akimrithi Mfaransa Pierre Luchan, kujiuzulu baada ya miezi miwili ya mkataba. Na katika Mwaka wa 2014, Shehata alifundisha Klabu ya Difaâ Hassani El Jadidi ya Morocco, na kisha Al Mokawloon Al Arab tena. Pia alifundisha Klabu ya Petrojet ya Misri mnamo mwaka wa 2017.
Shehata alipokea tuzo ya CAF ya Kocha Bora zaidi Barani Afrika kwa mwaka wa 2008, na aliorodheshwa kama Kocha Bora Barani Afrika katika orodha ya Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA) ya historia na takwimu za Soka, pamoja na kupewa taji la mtu wa mwaka Barani Afrika mnamo mwaka wa 2013, baada ya hapo aliheshimiwa wakati wa mkutano wa FIFA huko Brazil katika mwaka wa 2014.
Pia alitajwa kuwa mmoja wa makocha watano bora katika historia ya Bara la Afrika.
Vyanzo
Tovuti ya shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Tovuti ya Shirikisho la Soka la Misri.
Tovuti ya Mamlaka Kuu ya Habari ya Misri.