Nabawiya Musa ni Kiongozi wa Elimu ya Wasichana Huko Nchini Misri

Imetafsiriwa na/ Naira Abdelaziz
Imehaririwa na/ Nourhan Khaled
Nabawiya Musa amezaliwa tarehe 17, Desemba, 1886, katika mojawapo ya vijiji vya Mkoa wa Sharkia huko nchini Misri, kwa baba aliyekuwa Afisa katika Jeshi la Kimisri aliyetumwa nchini Sudan kabla ya kuzaliwa kwake kwa miezi miwili, na amekufa huko hivyo hajawahi kumwona na alikua yatima wa baba. Alivutiwa tangu utoto wake na elimu, lakini kutokana na mila na desturi kali zilizokuwepo wakati huo, wasichana hawakuruhusiwa kujiunga na shule kwa urahisi; kwa hivyo, amejifunza kusoma na kuandika nyumbani kwa msaada wa kaka yake mkubwa aliyeitwa "Mohamed", ambaye mara nyingi alikuwa akimfundisha masomo yake na alimfundisha kila kitu kwa mara ya kwanza.
Alisisitiza kujiunga na shule licha ya kukataa kwa familia yake, alikwenda shuleni kwa siri akijificha kwa kuvaa kama Mtumishi, na aliwasilisha nyaraka zake mwenyewe baada ya wizi wa muhuri wa mama yake ili kufanya sahihi ya mama yake ya kukubali kujiunga, mnamo mwaka 1901, Nabawiya aliingia kwenye idara ya nje ya Shule ya Sunia Kairo na akipata Cheti cha Elimu ya Kimsingi mnamo mwaka 1903, kisha akajiunga na Idara ya Walimu wa Shule ya Sunia na kumaliza mnamo 1906, na akateuliwa kama Mwalimu katika Shule ya Abbas ya Msingi ya Wasichana kwa mshahara wa pauni 6 kwa mwezi mmoja, ambayo ilikuwa nusu ya mshahara wa wanaume, kwa hivyo alitoa malalamiko kwa Wizara ya Elimu ambayo ilielezea tofauti hiyo ni cheti cha kidato cha sita, kwa hiyo alijiandaa kwa mtihani katika Shule ya Walimu wa Upili kutokana na kutokuwepo shule za sekondari za wasichana, na alipata cheti cha kidato cha sita mnamo mwaka 1907 licha ya kupingwa na wizara kwa sababu alikuwa msichana wa kwanza kupata cheti hicho, kisha alipata diploma ya walimu mnamo mwaka 1908, na alijaribu kupata shahada ya sheria, lakini hali ya uvamizi ilimzuia.
Nabawiya aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shule ya Msingi ya Mohammedia kwa Wasichana huko mkoani Fayoum mnamo mwaka 1909, na alifanikiwa katika kukuza elimu kwa wasichana huko Fayoum. Alikabiliana na changamoto kadhaa, lakini Ahmed Lotfi El-Sayed alimpendekeza kuwa Mkurugenzi wa Shule ya Walimu ya Mansoura, na alishinda nafasi ya kwanza katika mtihani wa uwezo wa walimu wa msingi. Chuo Kikuu cha kimisri cha Kibinafsi kilimteua kutoa mihadhara na Malak Hefny Nasif na Leila Hashem kwa ajili ya Elimu ya Wanawake wa tabaka la juu. Musa alianza kuandika makala katika magazeti kama "Misr Al-Fata" na "Al-Jarida" ambapo ndani yake amejadili masuala ya kijamii na elimu.
Nabawiya alihamishiwa Kairo na akateuliwa kuwa Naibu wa Walimu huko Bulak, kisha akapandishwa cheo kuwa Mkurugenzi wa Shule ya Walimu wa Wardian huko Alexandria, ambapo alikuwa Mkurugenzi wa kike wa Kwanza wa kimisri katika kipindi hicho kuanzia mwaka 1916 hadi 1920, na vilevile alishiriki katika maandamano ya wanawake mnamo mwaka 1919 pamoja na Safiya Zaghloul na Huda Shaarawi, na aliandika makala katika Magazeti kama "Al-Ahram," "Al-Siyasa," "Al-Balagh," na "Al-Mu'ayyad," ambapo alikosoa mifumo ya elimu na kwa kujibu waliompa likizo kulipwa. Alifanya mkataba na Jumuiya ya Maendeleo ya Wasichana huko Alexandria kuasisi Shule ya Msingi ya Wasichana na akachukua uongozi wake. Alikuwa ameandika kitabu chake "Mwanamke na Kazi" mnamo mwaka 1920, ambapo alitetea haki za wanawake. Pia aliandika kitabu cha kiada kinachoitwa "Matunda ya Maisha katika Elimu ya Wasichana," ambacho kilipitishwa na Wizara ya Elimu ya Kiarabu kwa kusomwa katika shule.
Mnamo mwaka wa 1923, alisafiri kwenda Roma na ujumbe wa wanawake wa kimisri kwenye Mkutano wa Wanawake wa Kimataifa. Baada ya kurudi Kairo, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wasimamizi katika Wizara ya Elimu. Kwa sababu ya ukosoaji wake kwa Wizara mnamo mwaka 1926, akitaka marekebisho ya programu za Wizara na kupunguzwa kwa shughuli za ukaguzi katika shule za wasichana kwa wanawake tu, bila wanaume au hata wanawake wa kigeni, Nabawiya hakupata majibu ya kuridhisha kutoka kwa malalamiko yake. Aliamua kuongeza suala hilo kwa Umma wa Kimisri, akachapisha makala katika gazeti la "Al-Siyasa Daily" chini ya kichwa cha habari "System of Girls' Education in England and Egypt". Hii ilisababisha kufutwa kazi kwake, lakini mahakama iliamua kuwa Wizara ililazimika kumlipa fidia ya pauni 550.
Nabawiya aliandika riwaya ya kihistoria iliyoitwa "Tawb Hatab" na tamthilia nzuri mnamo mwaka 1932. Alianzisha nyumba ya uchapishaji na jarida la kila wiki lililoitwa "Al-Fatah," ambalo lilidumu kwa miaka mitano hadi mwaka 1937. Pia alitunga diwani ya mashairi mnamo mwaka 1938. Nabawiya aliendelea kuwa na hamu ya elimu na akapewa jina la "Mpenzi wa Elimu." Alisimamia shule za kibinafsi kama Shule ya Wasichana ya Ashraf huko Alexandria, ambapo mwanasayansi wa nyuklia wa Misri Samira Moussa alihitimu. Pia alifungua tawi la shule hiyo huko Kairo na kuitoa shule ya Alexandria kwa Wizara ya Elimu mwaka 1946.
Nabawiya alishiriki katika mikutano mingi ya Kielimu na wanawake kwenye ngazi za ndani na kimataifa. Aliingiza njama ambazo zilimpelekea kufikishwa mahakamani, kufungwa, na kufungwa shule zake na jarida lake. Aliwafundisha lugha ya Kiarabu walimu wa kigeni na alishiriki katika kuanzishwa kwa Chama cha Wanawake wa Kimisri na mashirika mengi ya wanawake. Pia alikuwa miongoni mwa wanachama wa kwanza wa Chama cha Waandishi wa Habari.
Nabawiya alirekodi maisha yake yote katika kitabu chake "Tarikhi Bi Qalami" (Historia Yangu kwa Uandishi Wangu), akiwa mwanamke wa kwanza kuchapisha wasifu wake huko nchini Misri. Mfalme Fuad alimpa Tuzo ya Nile kama Mwajiriwa wa Kwanza wa Kike kuipokea, na jina lake lilitumiwa kuipa jina shule moja ya upili ya majaribio kwa wasichana huko Alexandria.
Tarehe 30, Aprili, 1951, amefariki dunia katika mazishi ya kuvutia katika Msikiti wa Sidi Abdelrazak Al-Wafa'i, ambapo wanawake na wasichana wengi wa kimisri walishiriki kwa idadi kubwa. Sala ilisaliwa juu ya mwili wake mtakatifu, kisha akapelekwa Kairo kwenye gari la wagonjwa. Mbele ya waombolezaji kulikuwa na Ahmed Morsi Badr Pasha, Waziri wa Elimu wa zamani, na wasimamizi wa elimu. Shule za Wasichana za Thaghr na wengi wa wazee, wanasayansi, na waandishi wa fasihi walimlilia.
Mwaka 1989, mashine ya kuchapisha ya Nabawiya Moussa ilipatikana ambayo alitumia kuchapisha machapisho yake wakati wa Ukoloni, wakati jengo la zamani la Shule ya Upili ya Wasichana ya Nabawiya Moussa ilipoangushwa huko Mahram Bek, Alexandria.
Vyanzo:
Tovuti ya Baraza la Kitaifa la Wanawake.
Gazeti la Al-Ahram.
Mratibu wa lugha ya kiswahili/ Tasneem Hamdy