Matarajio ya Kuimarisha Taswira Chanya ya Uwepo wa China Barani Afrika

Matarajio ya Kuimarisha Taswira Chanya ya Uwepo wa China Barani Afrika

Imetafsiriwa na: Ahmed Sayed 
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika muktadha wa ushirikiano kati ya Kituo cha Habari na Usaidizi wa Uamuzi na Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China huko Kairo, utafiti ulifanywa kwa jina "Matarajio ya Kuimarisha Taswira Chanya ya Uwepo wa China Barani Afrika", kama sehemu ya mradi wa utafiti "Athari za Uhusiano wa Kiuchumi kati ya China na Afrika kwenye Sekta ya Viwanda Barani Afrika".

Tangu mwaka 2000, China imekuwa mshirika muhimu katika juhudi za maendeleo ya Afrika kwa kufadhili miradi mbalimbali ya miundombinu ili kukidhi mahitaji ya bara hili. Mbinu ya ushirikiano wa manufaa ambayo China imepitisha imejikita pia kwenye matumizi ya nguvu laini ili kuimarisha uwepo wake barani Afrika. Aidha, kati ya miaka 2015 na 2016, ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika ulipata msukumo mkubwa kwa lengo la kufanikisha malengo ya maendeleo yaliyomo katika Ajenda ya Afrika 2063. Katika kipindi hiki, China ilifanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya kufadhili miradi ya maendeleo, huku mikataba mingi ya maelewano ikisainiwa kati ya Umoja wa Afrika na China, hasa katika nyanja za miundombinu kama barabara kuu, usafiri wa anga, na uunganishaji wa reli. Ushirikiano huu umefanya China kuwa mshirika mkuu wa maendeleo barani Afrika.

Kwa miongo kadhaa, Afrika imeathiriwa na changamoto za kihistoria ikiwa ni pamoja na unyonyaji wa rasilimali na kupuuzwa na mataifa ya Magharibi. Uhusiano wa kiuchumi kati ya Afrika na mataifa haya haukuweza kusaidia maendeleo ya bara kwa kiwango kinachohitajika, bali mara nyingi ulilenga kunufaisha uchumi wa Magharibi. Sambamba na hilo, Afrika inakabiliwa na changamoto kama ongezeko la idadi ya watu, ubora duni wa elimu, uhaba wa mafunzo ya ujuzi unaohitajika katika karne ya 21, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, viwango vya juu vya umaskini, na uhaba wa miundombinu bora.

China, kupitia mpango wake wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (Belt and Road Initiative - BRI), imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia Afrika kukabiliana na changamoto hizi kwa kujenga miundombinu ya kisasa, kuongeza fursa za ajira, na kuimarisha uzalishaji na biashara ya kimataifa. Mpango huu unalenga kuimarisha uwekezaji, kuboresha miundombinu, na kuimarisha biashara. Nchi nyingi za Afrika zimefaidika nao, na Misri ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kusaini mkataba wa kushiriki katika mpango huu. Mnamo mwaka 2015, Benki ya Uagizaji na Uuzaji ya China (EXIM Bank) ilisaini mkataba wa kufadhili miradi ya miundombinu nchini Misri yenye thamani ya takriban dola bilioni 10, ikihusisha sekta ya nishati, upanuzi wa bandari ya Alexandria, na uboreshaji wa reli za mijini. Kulingana na mshauri wa kiuchumi wa Umoja wa Afrika, mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja unatoa fursa kwa nchi wanachama wa Benki ya Uwekezaji ya Miundombinu ya Asia (AIIB) kupata mikopo ya maendeleo na misaada inayosaidia miradi ya miundombinu.

Katika miongo ya hivi karibuni, uwepo wa China barani Afrika umeongezeka kwa kasi, huku shughuli za Kichina zikihusisha sekta mbalimbali za uchumi. Taswira chanya ya uwepo wa China barani Afrika inaweza kuwa na mchango mkubwa katika mustakabali wa uhusiano kati ya pande hizi mbili. Katika muktadha huu, tafiti kama Afrobarometer zimejaribu kupima mtazamo wa Waafrika kuhusu ushiriki wa China katika bara lao. Kulingana na awamu ya sita ya utafiti huu, uliowahusisha watu kutoka nchi 36 za Afrika, takriban 25.8% ya wahojiwa waliona China kama nchi yenye ushawishi mkubwa zaidi, ikilinganishwa na 23.2% waliotaja Marekani.

Matokeo ya utafiti yalionesha kuwa takriban 60.6% ya wahojiwa wanaamini kuwa China ina athari chanya kwa nchi zao, huku 52.9% wakieleza kuwa misaada ya Kichina inakidhi mahitaji yao ya maendeleo. Aidha, 40.06% ya wahojiwa waliripoti kuwa China ina athari "kubwa" kwenye uchumi wao, huku 27.1% wakiona kuwa ina "baadhi" ya athari. Kwa ujumla, 67.9% ya wahojiwa walihusisha taswira chanya ya China barani Afrika na uwekezaji wake katika miundombinu, ubora na gharama nafuu ya bidhaa za Kichina, na ongezeko la biashara kati ya China na Afrika.

Chanzo: Tovuti ya Kituo cha Habari na Usaidizi wa Uamuzi - Ofisi ya Waziri Mkuu - Misri