Mapinduzi ya Julai 23 na Bara la Afrika

Mapinduzi ya Julai 23 na Bara la Afrika

Imeandikwa na: Menna Ashraf Rajab

Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Mapinduzi ya Julai 23, 1952, hayakuathiri Misri pekee, bali yalivutia bara zima la Afrika. Rais Gamal Abdel Nasser, kiongozi wa mapinduzi hayo, aliibua matumaini katika nchi za Afrika zilizokuwa zinatafuta kujikomboa kutoka kwa ukoloni wa Ulaya. Kujiunga kwa nchi za Afrika katika mapambano haya kulikuwa mwendelezo wa ukombozi wa Misri.

Mapinduzi yaliathiri kiwango cha kisiasa kwa njia zifuatazo:

1. Msaada kwa Harakati za Ukombozi: Misri iliunga mkono harakati za ukombozi na uhuru katika nchi za Afrika Mashariki kama vile Somalia, Kenya, Uganda, na Tanzania. Aidha, ilisaidia nchi za Afrika Magharibi na Kusini kama vile Nigeria, Ghana, na Congo kwa kuwapa silaha na pesa, pamoja na msaada wa kisiasa na kidiplomasia. Msaada huu ulisababisha uhuru wa nchi 17 za Afrika mnamo mwaka 1960.

2. Msimamo Dhidi ya Ubaguzi wa Rangi: Misri iliunga mkono watu wa Rhodesia Kaskazini (ambayo sasa ni Zambia) na Rhodesia ya Kusini (ambayo sasa ni Zimbabwe), hatima yao iliodhibitiwa na watu wachache wa Ulaya wenye ubaguzi wa rangi. Hali hii ilisababisha Misri kukatisha mahusiano ya kisiasa na Uingereza.

3. Kulaani Ubaguzi wa Rangi Afrika Kusini: Misri ililaani sera ya ubaguzi wa rangi iliyotekelezwa na utawala wa kibaguzi wa Ulaya nchini Afrika Kusini.

4.  Kauli Mbiu ya "Afrika kwa Waafrika": Misri iliinua kauli mbiu ya "Afrika kwa Waafrika" katika mkutano wa kwanza wa bara la Afrika mnamo tarehe Aprili 1958 kwenye mji mkuu wa Ghana.

5. Kujenga Umoja wa Afrika: Misri ilishiriki katika mkutano wa Mei 1963 mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ambapo Umoja wa Mataifa ya Afrika ulianzishwa. Rais Gamal Abdel Nasser aliongoza umoja huo mnamo mwaka 1964 na Misri iliiongoza tena mnamo mwaka 2019.

Sera ya mambo ya nje ya Misri imeweka idara ya Afrika kama kipaumbele chake cha kwanza, ikijumuisha ushirikiano, kuimarisha mahusiano, na kufuata mbinu na mikakati inayozingatia matukio ya sasa ya ndani, kikanda, na kimataifa.

Mchango wa Kiuchumi:

1. Kuanzisha Kambi za Kiuchumi: Misri ilianzisha kambi za kiuchumi ili kukabiliana na umaskini na unyonyaji wa rasilimali watu na maliasili ambayo ni sifa ya bara la Afrika.

2. Mfuko wa Kiufundi wa Misri: Misri ilianzisha Mfuko wa Kiufundi ili kushirikiana na nchi za Afrika kwa kuzipatia msaada kamili kwa kutuma wataalamu na mafundi na kuhakikisha ujenzi wa mabwawa ya maji.

Katika Uwanja wa Vyombo vya Habari:

1. Ofisi za Harakati ya Ukombozi: Misri ilifungua ofisi za vuguvugu la ukombozi wa Afrika mjini Kairo ili kueleza masuala ya watu wa Afrika kwa mtazamo wa dunia.

2. Matangazo ya Redio kwa Afrika: Misri ilianzisha matangazo ya redio kwa nchi za Kiafrika katika lugha nyingi za Kiafrika.

Mwishowe, jukumu la Misri linang'aa katika anga za Afrika, na kama Waswahili wanavyosema, "Muungano ni nguvu."