Kanisa Kuu la Mtakatifu Marko huko Abbasiya: Lulu ya Kanisa la Kikoptiki la Orthodox na Kivutio kwa Wakopti kutoka sehemu mbalimbali za Dunia

Kanisa Kuu la Mtakatifu Marko huko Abbasiya: Lulu ya Kanisa la Kikoptiki la Orthodox na Kivutio kwa Wakopti kutoka sehemu mbalimbali za Dunia

Imetafsiriwa na: Shrouk Mahmoud 
Imehaririwa na: Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr 

Huko mji mkuu wa Misri, hasa katika eneo la Abbasiya, Kanisa Kuu la Mtakatifu Marko linasimama kama alama muhimu ya kiroho na kihistoria, likiwa na hadithi za imani na utaifa kwenye kuta zake, na kwa hivyo kuwa kanisa kuu la pili kwa ukubwa katika ulimwengu wa Orthodox, na la zamani zaidi barani Afrika na Mashariki ya Kati, likiwa kivutio kwa Wakopti wote wanaoishi Misri na wale walioko nje ya nchi.

Kanisa hili linaitwa kwa jina la Mtakatifu Marko, mmoja wa wanafunzi wa kwanza waliosambaza Ukristo hadi sehemu za mbali zaidi za dunia. Kwa mujibu wa simulizi, Mtakatifu Marko alizaliwa Yerusalemu, lakini safari yake ya kuhubiri ilimpeleka Misri, ambapo alikaa huko Aleksandria, mji ambao baadaye ulikuwa makao makuu ya Kipapa, na chimbuko la Kanisa la Kikoptiki la Orthodox.

Kanisa kuu halikuwa mradi wa kidini tu, bali pia lilikuwa na maana ya kihistoria ya kitaifa, iliyoonyeshwa kwa kuunga mkono uongozi wa kisiasa wa wakati huo. Katika tukio la kihistoria lisilosahaulika, Rais wa zamani Gamal Abdel Nasser alichangia kiasi kikubwa cha fedha mnamo mwaka 1960 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa kuu, na yeye mwenyewe aliweka jiwe la msingi mnamo Julai 24, 1965, mbele ya Mtawala Hella Selassie wa Ethiopia na Papa Kyrillos, Papa wa Alexandria na Patriaki wa Injili ya Marko wakati huo.

Ubunifu wa kanisa kuu ulilenga kuakisi roho ya imani na umuhimu wa msalaba katika Ukristo, huku jengo likiwa na umbo la msalaba. Ubunifu huu ulikuwa kazi ya wahandisi Dkt. Awad Kamel na Salim Kamel Fahmy, walioshinda shindano la kuchora na kubuni kanisa. Utekelezaji wa ujenzi ulisimamiwa na Dkt. Michel Bakhoum, mmoja wa wahandisi mashuhuri wa ujenzi nchini Misri, huku utekelezaji ukiwekwa mikononi mwa kampuni ya "Nile General for Reinforced Concrete (SIBCo)", ili kujenga mojawapo ya majengo makubwa ya kidini katika eneo hilo.

Kanisa kuu haliwezi kuonekana kama ukumbi mkubwa tu wa sala, bali pia lina makanisa mengi na huduma nyingine, ikiwemo makanisa mawili chini ya kanisa kuu yanayoitwa "Bikira Maria", pamoja na makanisa ya "Bikira Maria na Anba Rowais", "Bikira Maria na Anba Bishoy", na "Anba Antonious" lililoko katika makao ya Kipapa. Aidha, kuna makanisa yenye majina ya Mtakatifu Maurice, Mtakatifu Verena, Anba Bola, na Anba Samuel. Zaidi ya hayo, kuna majengo ya kiaskofu yaliyopangwa maalum kwa ajili ya kutoa huduma za kidini na kijamii, huku kuta zake zikihifadhi kumbukumbu nyingi za sherehe, ziara, na matukio ya kihistoria.

Kanisa Kuu la Mtakatifu Marko si jengo tu, bali ni kumbukumbu hai ya historia ya Kanisa la Kikoptiki la Orthodox, na ushahidi wa uhusiano kati ya dini na taifa. Kila mwaka, makundi ya watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia hukusanyika hapo, kushuhudia ukuu wake, kuikumbuka roho ya Mtakatifu Marko, na kuimarisha uaminifu wao kwa urithi wa imani isiyo na mipaka.

Kanisa Kuu la Mtakatifu Marko huko Abbasiya, Kairo linabaki kuwa jengo linaloakisi imani, historia, na umoja wa kitaifa… alama ya kiroho inayovuka mawe na paa ndefu, ikigusa mioyo ya waumini kila kona ya dunia.