Dkt. Ragaa Magdy: Nguvu ya kuendesha mabadiliko endelevu katika nyanja za kitaaluma, ujasiriamali na mipango ya kimataifa

Dkt. Ragaa Magdy: Nguvu ya kuendesha mabadiliko endelevu katika nyanja za kitaaluma, ujasiriamali na mipango ya kimataifa

Imetafsiriwa na: Alaa Abdelghani
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Dkt. Ragaa Magdy ni kiongozi mwenye nguvu anayefanya maendeleo makubwa katika masomo, ujasiriamali na juhudi za kimataifa za uhimilivu. Akiwa na historia tajiri katika kemia ya uchambuzi wa dawa, anachanganya utaalamu wake wa kisayansi na shauku ya kuendeleza suluhisho endelevu na kuwezesha jamii.

Safari ya kielimu ya Dkt. Magdy ni mfano bora wa kujitolea na ubora. Ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Kemia ya Uchambuzi wa Dawa Endelevu na ya Kijani kutoka Chuo Kikuu cha Ain Shams. Michango yake inaonekana kupitia uandishi wa makala 14 za kimataifa zinazolenga kemia ya kijani na uhimilivu. Kwa sasa, Dkt. Magdy ni profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Kanada mjini Kairo, ambapo anawafundisha na kuwaongoza vizazi vijavyo vya wafamasia.

Mbali na mafanikio ya kielimu, Dkt. Magdy, Mhitimu wa kundi la nne la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, ni mjasiriamali aliyefanikiwa. Yeye ndiye Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa RUJA Natural Cosmetics and Skincare Products, kampuni inayotanguliza bidhaa asili, endelevu na zenye ufanisi. Ujuzi wake wa kibiashara umeimarishwa na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) kutoka Shule ya Biashara ya Brooklyn.

Ushawishi wa Dkt. Magdy unaenea katika jukwaa la kimataifa. Anafanya kazi pia kama mshauri wa UN Women kuhusu Kanuni za Kuwawezesha Wanawake na ni mwanachama wa Kamati ya Uendelevu ya Michezo ya Sharjah katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Uongozi wake wa kimataifa unaonekana pia kupitia jukumu lake kama mshauri, mtathmini na mwelekezi wa Changamoto ya Sera na Mijadala ya 2024 katika Jukwaa la Kimataifa la Chakula (WFP/FAO), akichangia katika mipango ya hali ya hewa. Pia alishiriki kikamilifu katika COP27.

Zaidi ya hayo, Dkt. Magdy ni mkufunzi na mwelekezi aliyejitolea. Anaongoza mpango wa Mifumo ya Huduma za Afya Endelevu, akitoa mafunzo kuhusu ujasiriamali, uhimilivu na usawa wa kijinsia. Katika Chuo Kikuu cha Ahram Kanada mjini Kairo, anahudumu kama afisa wa Mfuko wa Ubunifu na Biashara Changiza, akiwaongoza wanafunzi kubadilisha mawazo yao kuwa biashara changiza zinazoweza kufanya kazi. Kujitolea kwake katika kukuza ujasiriamali pia kunadhihirika kupitia jukumu lake kama mwelekezi katika mpango wa MicroMentor (Mercy Corps), ambapo anaongoza wajasiriamali katika masuala ya kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na fedha za Tabianchi.

Michango ya Dkt. Magdy imetambuliwa kupitia usomi na vyeti vingi, ikiwemo Cheti cha Uongozi kutoka mpango wa Wanawake Wanaongoza Misri wa Chuo cha Mafunzo cha Kitaifa na cheti cha Balozi wa Maabara ya Kijani kutoka shirika la My Green Lab.

Dkt. Ragaa Magdy ni kiongozi wa kipekee mwenye sura nyingi, ambaye kazi yake inajumuisha masomo, ujasiriamali na mipango ya kimataifa. Shauku yake ya uhimilivu, pamoja na utaalamu na kujitolea kwake, inamweka kama nguvu muhimu inayoendesha mabadiliko chanya nchini Misri na duniani kote.