Adel Al-Mahrouqi: Kutoka Shauku ya Kompyuta hadi Mwangaza wa Uandishi wa Habari - Hadithi ya Shauku Isiyozimika

Adel Al-Mahrouqi: Kutoka Shauku ya Kompyuta hadi Mwangaza wa Uandishi wa Habari - Hadithi ya Shauku Isiyozimika

Imetafsiriwa na: Amira Reyad Bekhit
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Safari ya Adel Al-Mahrouqi ni ushahidi wa nguvu ya mtu kufuata shauku yake ya kweli, hata ikihitaji mabadiliko makubwa katika mwelekeo wake, baada ya kuazimia mwanzoni kufuata njia ya sayansi ya kompyuta. Maisha yake yalichukua mkondo usiotarajiwa katika mwaka wake wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Marekani, Kairo, alipogundua shauku yake kubwa kwa televisheni. Ugunduzi huo ulimshawishi kufanya uamuzi wa ujasiri wa kuacha shahada ya sayansi ya kompyuta aliyokuwa karibu kuikamilisha, na kujitumbukiza moja kwa moja katika dunia ya utayarishaji wa televisheni ya kuvutia.

Kuvutiwa kwake na mambo tata ya televisheni kuanzia kazi ya kamera, ufuatiliaji wa moja kwa moja, hadi utayarishaji, uhariri, uandishi na matangazo ya satelaiti, ndiyo ulichochea shauku yake. Safari ya taaluma ya Adel ilianza mnamo mwaka 2005 katika ofisi ya habari ya NHK ya Japan, Cairo, ambapo alijitumbukiza haraka katika ulimwengu wenye mabadiliko ya haraka wa habari za moja kwa moja, na alishuhudia umuhimu wa matukio muhimu ya kisiasa kama uchaguzi wa bunge na uchaguzi wa kwanza wa urais wenye wagombea wengi nchini Misri. Hata mwanzoni mwa maisha yake ya kazi, Adel alionyesha kipaji cha kipekee na alipata majukumu ya kuandika hotuba kwa maafisa wakuu, akiwemo Waziri Mkuu wa Misri wa wakati huo, Ahmed Nazif.

Safari ya taaluma ya Adel Al-Mahrouqi ina uzoefu mkubwa wa kuripoti habari katika nchi 16, katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Kazi yake imempeleka kutoka nchi za Ghuba ya Kiarabu, kupitia nchi mbalimbali za Kiarabu hadi Algeria, kisha hadi maeneo ya Palestina yaliyokaliwa, na kutoka kusini mwa Misri hadi Ethiopia. Amepitia baadhi ya mazingira yenye changamoto na hatari zaidi katika eneo hilo, ikiwemo kushuhudia mapigano ya risasi na mashambulizi ya anga nchini Lebanon, na kuripoti uchaguzi wa urais nchini Iran.

Kujitolea kwake kwa uandishi wa habari kunadhihirika kwa utayari wake wa kuvumilia usiku mrefu wa kukesha katika ofisi mbalimbali kote katika eneo hilo. Yeye yuko tayari kuwa wa kwanza kufika mahali popote tukio linapotokea. Shauku ya Adel ya kukabiliana na changamoto zisizotarajiwa na kutoa maudhui ya kuvutia kwa hadhira ya vipindi vyake vya moja kwa moja vya mijadala ni sifa kuu zinazotambulisha safari yake ya kazi. Historia ya Adel Al-Mahrouqi iliyojaa mafanikio inafungua njia kwa sura mpya, ambapo anakabiliana na changamoto zijazo kwa uwezo uleule wa kujiendeleza, kubadilika, na shauku ya dhati kwa uandishi wa habari iliyotambulisha safari yake.