Mahusiano ya Misri na Senegal

Mahusiano ya Misri na Senegal

Imetafsiriwa na: Ibrahim El-Sqqa
Imehaririwa na:  Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Mahusiano ya Kisiasa:

Misri ilikuwa mstari wa mbele katika nchi zilizoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Senegal mara tu baada ya uhuru wake, kama ilivyoanza mnamo tarehe 4/4/1960, kutokana na nguvu ya mahusiano yaliyokuwa kati ya Rais wa Misri Gamal Abdel Nasser na Rais wa Senegal Leopold Senghor, na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ikawa nchi ya pili kutambua uhuru wa Jamhuri ya Senegal baada ya Ufaransa.

Mahusiano kati ya nchi hizo mbili yanaendelea kukua kwa viwango vyote, na kuna maono yanayopatana kuhusu masuala ya kimataifa. Pia, nchi hizi zinashirikiana katika majukwaa ya kimataifa na kikanda, hususan Umoja wa Mataifa, Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, Umoja wa Afrika, na eneo la Sahel na Jangwa la Sahara, kulingana na mpango wa "NEPAD" kwa maendeleo barani Afrika.

Misri yashiriki katika mpango wa kimataifa wa “Dakar” kuhusu amani na usalama barani Afrika kila mwaka. Mpango huu ulianzishwa na Rais wa Senegal, Macky Sall, mnamo mwaka 2014. Ushiriki wa Misri ulilenga kuunga mkono juhudi za pamoja za Afrika kupambana na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika. Mpango huu unalenga kutafuta njia za kupambana na ugaidi barani Afrika, na uwezekano wa kuweka mikakati yenye ufanisi kukabiliana na tukio hilo na kueneza amani barani humo. Vilevile, mpango huu unahusisha ubadilishanaji wa maono kati ya madola mbalimbali ya kikanda na kimataifa yanayoshughulikia masuala ya amani na usalama barani Afrika. Pia, Misri ilishiriki kwenye mkutano wa kilele wa 15 wa Shirika la Kimataifa la Ufaransa uliofanyika katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, mnamo tarehe Novemba 2014.

Ziara za pamoja kati ya Misri na Senegal:

Mnamo tarehe Januari 2023, Rais wa Misri Abd El-Fattah El-Sisi alipokea simu kutoka kwa mwenzake wa Senegal, Macky Sall, ambapo walijadili maandalizi ya Mkutano wa Kilele wa Afrika uliopangwa kufanyika mnamo tarehe Februari 2023. El-Sisi alimpongeza Rais Sall kwa uongozi wake bora wa Umoja wa Afrika katika mwaka uliojaa changamoto za kimataifa na za kikanda, na athari zake kwa Afrika. Kwa upande wake, Sall alitoa shukrani zake kwa msaada wa Misri katika kipindi cha uongozi wake, akisisitiza juhudi za Misri katika kuimarisha masilahi ya pamoja ya Afrika na kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazoikabili bara hilo. Vilevile, walijadili faili muhimu zaidi na masuala yenye maslahi ya pamoja.

Mnamo tarehe Februari 2022, El-Sisi alikutana na Rais Sall kwenye Mkutano wa Kilele wa Ulaya na Afrika, ambapo walijadili kuimarisha mahusiano ya pande mbili kati ya nchi hizo.

Mnamo Januari 29, 2022, Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sisi na Rais wa Senegal Macky Sall walifanya mazungumzo kuhusu mahusiano ya pande mbili, masuala ya kupambana na ugaidi, itikadi kali, na juhudi za kukabiliana na janga la COVID-19.

Katika mazungumzo hayo, Rais Al-Sisi alionyesha uungaji mkono wake kwa Rais Sall, ambaye alikuwa akijiandaa kuchukua urais wa Umoja wa Afrika, akisisitiza imani yake katika uongozi wa Rais Sall katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Afrika, ikiwemo janga la COVID-19 na ugaidi. Aidha, Rais Al-Sisi alitoa shukrani kwa ushirikiano kati ya Misri na Senegal katika nyanja mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Kwa upande wake, Rais Sall alithamini mahusiano ya kipekee kati ya Senegal na Misri, akionesha nia yake ya kuimarisha mahusiano hayo, hasa katika nyanja za biashara na uchumi, na kutoa shukrani kwa shughuli za mashirika ya Misri nchini Senegal. Vilevile, marais hao walisisitiza umuhimu wa kuzidisha ushirikiano na utaratibu wa kukabiliana na changamoto za kikanda, hasa suala la Bwawa la Ethiopia, wakikubali umuhimu wa utaratibu na ushauri wa pamoja katika kufuatilia maendeleo.

Mnamo tarehe Mei 19, 2021, wakati wa mkutano wao, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi na Rais wa Senegal Macky Sall walisisitiza mahusiano yenye ufanisi kati ya Misri na Senegal na walionesha utayari wao wa kukuza ushirikiano wa pamoja katika nyanja za kibiashara, uwekezaji, kuimarisha miundombinu, na kujenga uwezo. Mkutano huo ulifanyika baada ya ziara ya Rais El-Sisi mjini Dakar mnamo tarehe Aprili 2019.

Mnamo tarehe Desemba 12, 2019, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi alipokea mwenzake wa Senegal, Macky Sall, pembezoni mwa Jukwaa la Amani na Maendeleo Endelevu la Aswan. El-Sisi alisifu mahusiano thabiti na Senegal, akionesha utayari wa Misri kupanua wigo wa ushirikiano wa pamoja katika nyanja za biashara, uwekezaji, na maendeleo ya miundombinu, kama sehemu ya ziara yake ya mafanikio mjini Dakar mnamo tarehe Aprili 2019. Kwa upande wake, Macky Sall alisifu maendeleo endelevu ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kutoa shukrani zake kwa Misri na uongozi wake, akisisitiza umuhimu wa kushiriki kwa Misri katika Jukwaa la Aswan ili kuunga mkono jukumu lake katika kufanikisha maendeleo na amani barani Afrika.

Mkutano huo pia ulijadili ushirikiano katika kupambana na ugaidi na itikadi kali, huku Misri ikielezea matarajio yake ya kuimarisha ushirikiano na Senegal katika kueneza fikra za Uislamu wa wastani, pamoja na kuimarisha jukumu la ujumbe wa Al-Azhar nchini Senegal. Marais hao pia walijadili masuala ya bara zima na walikubaliana kuendelea kushauriana na kuratibu kuhusu maendeleo ya kanda, hasa yale yanayohusu Afrika Magharibi.

Mnamo tarehe Agosti 25,  2019, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi aliwapokea viongozi wa Rwanda, Senegal, Afrika Kusini, Burkina Faso, na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika pembezoni mwa mkutano wa Kundi la Saba (G7) huko Biarritz, Ufaransa. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuratibu na kushauriana ili kuunganisha ujumbe wa Afrika wakati wa mkutano huo, na kusisitiza ushirikiano wa haki na washirika wa kimataifa, pamoja na kuangazia vipaumbele vya maendeleo vya bara hilo.

Marais walioshiriki walitoa shukrani zao kwa mpango wa Misri wa kuratibu misimamo ya Afrika, wakisisitiza umuhimu wa muungano wa bara na uhuru wa biashara ndani kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika. Mnamo tarehe Juni 18, 2019, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi alihudhuria mkutano mdogo wa uratibu wa viongozi wa Afrika mjini Osaka, akiwa na marais wa Afrika Kusini na Senegal. Lengo lilikuwa ni kuunganisha misimamo ya nchi za Afrika ili kuimarisha maslahi yao katika mikutano ya Kundi la Ishirini (G20), wakinufaika na uanachama wa Afrika Kusini kwenye kundi hilo, pamoja na jukumu la Senegal katika Kamati ya NEPAD, na uenyekiti wa Misri katika Umoja wa Afrika.

Mnamo tarehe Aprili 12, 2019, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi alitembelea Senegal ambapo alipokelewa na Rais Macky Sall. Wakati wa ziara hiyo, pande zote mbili zilisisitiza uhusiano wa kina wa kihistoria na umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali, hasa za kiuchumi na kibiashara, pamoja na kunufaika na uzoefu wa Misri katika maendeleo ya miundombinu na maeneo mengine ili kuunga mkono mpango wa maendeleo wa Senegal. Rais El-Sisi alielezea furaha yake kwa ziara hiyo na kumpongeza Rais Sall kwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili, akisisitiza mahusiano ya kidugu kati ya nchi hizo mbili katika siasa, utamaduni, na dini, pamoja na kufanana kwa misimamo yao katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Mkutano huo pia ulijadili ushirikiano katika kupambana na ugaidi na kukuza mawazo ya Uislamu wa wastani, huku wakisisitiza umuhimu wa kamati ya pamoja ya Misri na Senegal ili kuimarisha na kuendeleza mahusiano hayo. Rais El-Sisi alimkaribisha Rais wa Senegal kufanya ziara nchini Misri. Mahusiano kati ya Misri na Senegal umeshuhudia mipango kadhaa ya kuimarisha ushirikiano katika miaka ya hivi karibuni.

Mnamo tarehe Mei 2023, Balozi wa Misri mjini Dakar alishiriki katika kongamano kuhusu Eneo Huru la Biashara barani Afrika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika. Pia alihudhuria mkutano ulioitishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal ili kuangazia mafanikio ya Senegal wakati wa uenyekiti wake wa Umoja wa Afrika.

Mnamo tarehe Desemba 2022, mkutano kati ya Jumuiya ya Vijana wa Vyama vya Kisiasa vya Misri na Balozi wa Senegal mjini Kairo ulisisitiza umuhimu wa mahusiano ya pande mbili, wakionesha kina chake na matarajio ya kuimarishwa kwa ushirikiano huo katika siku zijazo.

Mnamo tarehe Novemba 2021, Dakar iliandaa duru ya mashauriano ya kisiasa iliyoangazia njia za kuimarisha mahusiano, hasa katika nyanja za uwekezaji, biashara ya kibiashara, na kupambana na ugaidi, huku ikisisitiza uratibu kuhusu masuala ya amani na usalama ya Kiafrika na Kimataifa.

Mnamo tarehe Februari 2020, Jenerali Mohamed Zaki, Waziri wa Ulinzi wa Misri, alikutana na Waziri wa Vikosi vya Kijeshi wa Senegal, Sidiki Kaba, ambapo walionesha dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiusalama kwa manufaa ya pande zote.

Mnamo tarehe Novemba 2017, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alishiriki katika Jukwaa la Dakar kuhusu Amani na Usalama, na mnamo tarehe Oktoba mwaka huo huo, Mshauri wa Rais wa Senegal kuhusu Masuala ya Kidini alitembelea Misri kujadili kuimarisha ushirikiano na kuiomba Misri kushiriki katika jukwaa hilo.

Mnamo tarehe Septemba 2017, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alibeba ujumbe kutoka kwa Rais El-Sisi kwenda kwa Rais wa Senegal kuhusu kuimarisha uhusiano wa pande mbili na msaada wa Senegal kwa mgombea wa Misri katika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO.

Mnamo tarehe Machi 2014, Mansour Niasse, mjumbe maalumu wa Rais wa Senegal, alitembelea Misri ambapo alipokelewa na Rais wa zamani wa Misri, Adly Mansour, na kumkabidhi mwaliko wa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Nchi za Kifaransa (Francophonie) nchini Senegal. Niasse alitoa ujumbe wa shukrani na mshikamano kutoka kwa Rais wa Senegal kwa Misri, akipongeza msaada wa kihistoria wa Misri na jukumu la Al-Azhar katika kueneza elimu na Uislamu nchini Senegal. Pia alitoa pole kwa waathiriwa wa ugaidi nchini Misri na kueleza msaada wa Senegal kwa kurudi kwa Misri katika Umoja wa Afrika.

Mnamo tarehe Novemba 2013, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alitembelea Senegal, ambapo alijadili na mwenzake wa Senegal kuhusu mahusiano ya pande mbili na masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja.

Mnamo mwaka 2012, Rais wa Senegal, Macky Sall, alihudhuria Mkutano wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu nchini Misri. Mnamo tarehe Mei 2011, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alitembelea Senegal.

Mnamo tarehe Novemba 2008, Waziri wa zamani wa Umwagiliaji na Rasilimali za Maji wa Misri alishiriki katika mkutano wa Afrika kuhusu kupambana na mmomonyoko wa pwani nchini Senegal. Mnamo tarehe Machi 2008, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Misri alihudhuria mkutano wa kilele wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu nchini Senegal.

Mnamo tarehe Oktoba 2005, Waziri wa Masuala ya Wasenegali wanaoishi ughaibuni alitembelea Misri, hatua inayodhihirisha kuendelea kwa kubadilishana na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali na ngazi tofauti.

Ushirikiano katika Sekta ya Utalii na Mambo ya Kale: Misri na Senegal zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja za utamaduni na urithi, ambapo Misri inachangia katika ukarabati wa urithi wa kitamaduni wa Senegal na maandiko ya Kiislamu, huku ikitoa nakala za kitamaduni za mali za kale za Misri kwa ajili ya kuoneshwa katika Jumba la Makumbusho la Ustaarabu wa Afrika.

Mnamo tarehe Desemba 2, 2022, Balozi wa Senegal mjini Kairo alisifu maendeleo makubwa katika utalii wa tiba nchini Misri, akibainisha umuhimu wa sekta hii katika kuvutia watalii na kutoa huduma za matibabu bora kutokana na wataalamu wenye sifa na hali ya hewa ya joto. Pia alihimiza kupanua wigo wa utalii wa tiba kupitia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kupanga ziara za kubadilishana uzoefu. Mnamo tarehe Julai 12, 2016, Waziri wa Utalii na Usafiri wa Anga wa Senegal alitembelea Misri kwa ajili ya kujadili kuimarisha ushirikiano wa utalii kati ya nchi hizo mbili.

Umeme na Nishati:

Mnamo tarehe Februari 3, 2023, Waziri wa Umeme na Nishati Mbadala wa Misri, Dkt. Mohamed Shaker, alikutana na Waziri wa Nishati wa Senegal, Aïssatou Sophie Gladima, pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Afrika uliofanyika Dakar. Katika mkutano huo, walijadili njia za kuimarisha ushirikiano wa baadaye katika sekta ya umeme na nishati, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa sekta binafsi katika eneo hili. Shaker alieleza juhudi zilizofanywa na Misri kushinda changamoto katika sekta ya umeme, na kusifu jukumu la uongozi wa kisiasa wa Misri katika kusaidia sekta hii muhimu. Pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Misri na nchi za Afrika, huku akionesha utayari wa Misri kutoa msaada na kubadilishana uzoefu na Senegal.

Wakati wa mkutano huo, Dkt. Shaker pia alishiriki kwenye kikao kuhusu suluhisho za kifedha ili kuharakisha upatikanaji wa nishati barani Afrika. Alizungumza juu ya mafanikio ya Misri katika kuongeza uwezo wake wa uzalishaji wa umeme kutoka gigawati 20 hadi gigawati 60 ndani ya miaka tisa, akibainisha kwamba Misri inazingatia mpito kuelekea nishati safi. Alisema kuwa Misri imeongeza gigawati 28 za nishati mbadala kwenye gridi yake ya umeme. Pia alitaja kwamba Misri imesaini makubaliano matatu ya miradi ya nishati ya upepo kwa lengo la kuongeza gigawati 28 zaidi kwa bei za ushindani, jambo ambalo litasaidia kufikia lengo la kuongeza sehemu ya nishati mbadala hadi 42% ifikapo mwaka 2030.

Ushirikiano katika Sekta ya Usafiri:

Mnamo tarehe Desemba 23, 2023, Balozi Khaled Aref, Balozi wa Misri mjini Dakar, alihudhuria sherehe ya uzinduzi wa safari ya kwanza ya ndege ya kampuni ya Air Cairo kutoka Dakar hadi Kairo. Hii ni sehemu ya juhudi za Misri kuimarisha ushirikiano wa anga na nchi za Afrika na kupanua mtandao wake wa safari za moja kwa moja. Mhandisi Hussein Sharif, Mwenyekiti wa Air Cairo, alikuwa kwenye ndege ya kwanza kuelekea Dakar, na sherehe hiyo ilihudhuriwa pia na mwakilishi wa Waziri wa Usafiri wa Anga, Omar Dia, mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya usafiri wa angani ya Senegal (ANACIM), Mansour Sy, na viongozi wa miji kama Omar Baldé wa Thies, pamoja na wawakilishi wa kampuni za utalii nchini Senegal na wanajamii wa Misri.

Mawasiliano na Teknolojia ya Habari:

Mnamo tarehe Mei 29, 2023, Balozi wa Jamhuri ya Misri nchini Senegal, Khaled Aref, alisisitiza umuhimu wa juhudi zinazofanywa na kampuni za Misri katika sekta ya teknolojia ya habari na huduma za kidijitali kufungua masoko mapya nje ya nchi, hasa barani Afrika. Alizungumzia ushiriki wa Misri katika maonesho ya kila mwaka ya elimu ya mtandao (Dakar) na kueleza kuwa juhudi hizi zinaendana na malengo ya serikali ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi na nchi za Afrika, pamoja na mpango wa "GO TO Africa," ulioanzishwa na chumba cha biashara cha teknolojia ya habari na mawasiliano ya Misri mnamo tarehe Juni 2022. Alisema kuwa ushiriki wa Misri katika maonesho haya ni fursa nzuri ya kujifunza mitindo mipya katika sekta ya elimu ya mtandao na kuimarisha ushirikiano na mashirika na kampuni nyingi za kimataifa kutoka nchi zaidi ya 20.

Senegal, kutokana na elimu yake ya juu, inajitokeza kama mshirika muhimu wa Misri katika sekta ya elimu, hasa kupitia jukumu muhimu la Al-Azhar katika kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili. Misafara ya kidini kutoka Al-Azhar nchini Senegal ina wataalamu 37, ikiwa na mipango ya kuongezeka hadi 40, kwa lengo la kukabiliana na mitazamo mingine ya kidini na kueneza Uislamu wa wastani. Senegal inashika nafasi ya pili baada ya Sudan kwa idadi ya wanafunzi wanaosoma katika Al-Azhar, ambapo takriban wanafunzi 600 wa Senegal wanajifunza, na karibu 30% yao wanapata ufadhili wa masomo.

Alexandria inakaribisha "Chuo cha Senghor," taasisi ya elimu na utamaduni ya kimataifa inayoshughulika na maendeleo ya Afrika, iliyoanzishwa mwaka 1989, ambayo ina maana kubwa ya kisiasa na kitamaduni, ikitokana na ndoto ya Rais wa zamani wa Senegal, Léopold Sédar Senghor, ya kuanzisha taasisi ya elimu ya Kiafrika inayochangia katika maendeleo na uboreshaji wa bara.

Misri ilihudhuria maonesho ya kila mwaka ya elimu ya mtandao mjini Dakar mnamo tarehe Mei 29, 2023, kwa kuungwa mkono na wizara za elimu na uchumi wa kidijitali, huku ikiwa na wawakilishi kutoka kampuni 12 za Misri katika sekta ya teknolojia ya habari, ili kuchunguza fursa za ushirikiano na kusaidia bidhaa za Misri nchini Senegal na Gambia, hatua inayosaidia kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu ya mtandao.

Mnamo tarehe Januari 19, 2022, Dkt. Shawki Allam, Mufti wa Jamhuri na Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Taasisi na Mifumo ya Fatwa duniani, alimpokea Dkt. Aboubacar Sarr, Balozi wa Senegal mjini Kairo, kujadili njia za kuimarisha ushirikiano wa kidini kati ya Misri na Senegal. Mufti alithibitisha kuwa Dar al-Ifta ya Misri iko tayari kutoa msaada wa kisayansi na wa kidini kwa Waislamu wa Senegal, hasa katika mafunzo ya imamu ili kukabiliana na fikra kali. Balozi wa Senegal alisifu juhudi za Dar al-Ifta ya Misri katika kupambana na itikadi kali na ugaidi, na kueleza hamu ya nchi yake ya kunufaika na uzoefu huo, hasa katika mafunzo ya imamu.

Mnamo tarehe Oktoba 12, 2021, Baraza Kuu la Utamaduni la Misri, kwa kushirikiana na Sekta ya Mahusiano ya Kimataifa ya Utamaduni, lilifanya jioni ya "Misri/Senegal... Mahusiano ya Kitamaduni" kama sehemu ya mpango wa kuimarisha mahusiano ya kitamaduni, ulioandaliwa na Wizara ya Utamaduni ya Misri.

Misri ilishiriki katika kikao cha 11 cha Kamati ya Kudumu ya Habari na Masuala ya Kitamaduni ya Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu mnamo tareh Mei 13, 2018 mjini Dakar, chini ya kauli mbiu ya Kusaidia Amani na Maendeleo kupitia Elimu na Utamaduni, kwa kuzingatia azimio la Mkutano wa Kilele wa Kiislamu wa tatu mnamo mwaka 1981 mjini Makkah, kwa lengo la kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari na utamaduni katika ulimwengu wa Kiislamu na kutambulisha masuala makubwa yanayowakabili.

Mnamo tarehe Novemba 2017, Rais wa Chuo Kikuu cha Ain Shams, Sheikh Tjan Gueye, alipokea mshauri wa kitamaduni kutoka Ubalozi wa Senegal, ili kujadili kuimarisha ushirikiano kati ya Misri na Senegal katika nyanja za ubadilishanaji wa wanafunzi na tafiti za kisayansi. Waziri wa Elimu wa Misri, Dkt. Tarek Shawki, alitembelea Senegal mnamo tarehe Machi 16, 2017 ili kushiriki katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Kuendeleza Elimu Barani Afrika.

Mnamo tarehe Desemba 14, 2016, Rais wa Misri alimpokea Waziri wa Elimu wa Senegal, aliyetoa ujumbe kutoka kwa Rais wa Senegal ukiashiria hamu ya nchi yake kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na Misri katika nyanja mbalimbali.

Mnamo tarehe Aprili 2005, Waziri wa Awqaf wa zamani wa Misri alifanya ziara nchini Senegal, akionesha dhamira ya kuendelea na kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.