Nurella Turambetov… Mwalimu anayesambaza thamani za uvumilivu kupitia elimu
Imetafsiriwa na: Mohamed Ahmed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika moyo wa mji mkuu wa Uzbekistan, Tashkent, Nurella Turambetov, profesa mashuhuri wa masomo ya dini, anaendelea na jukumu lake tukufu la kulea kizazi kipya kinachoamini katika mazungumzo, uwazi na kuishi pamoja kwa amani. Kupitia uzoefu wa miaka mingi katika kufundisha, kufanya utafiti na kutoa mafunzo, Turambetov ameonesha kwamba elimu inaweza kuwa chombo chenye nguvu cha kusambaza amani na kujenga madaraja kati ya tamaduni na dini.
Turambetov ana shahada ya uzamili katika masomo ya dini kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Kimataifa cha Uzbekistan, ambako kwa sasa anafanya kazi kama profesa chini ya Kiti cha UNESCO cha Masomo ya Ulinganisho wa Dini za Dunia. Anafahamika kwa mbinu yake ya kiubunifu ya kielimu inayotegemea ujifunzaji shirikishi, kuhimiza mtazamo chanya na kuzingatia tofauti binafsi kati ya wanafunzi, jambo lililomfanya asifiwe na wanafunzi wake pamoja na wenzake wa kazi.
Mchango wake haukuzuilika tu katika elimu ya vyuo vikuu, bali pia alishikilia nyadhifa za uongozi na utawala kama vile msaidizi wa mkurugenzi wa kitengo cha uzamili katika Chuo cha Kiislamu, ambapo alichangia katika kuendeleza mitaala mbalimbali na kukuza wingi na ushirikishwaji ndani ya taasisi hiyo ya kielimu. Pia alifanya kazi kama mkufunzi wa walimu, jambo linaloonyesha dhamira yake ya dhati ya kukuza uwezo wa walimu.
Turambetov amehusiana na majukumu mengi yaliyohusisha tafsiri ya papo kwa hapo na utafiti wa kisayansi, ambapo alianza safari yake kama msaidizi wa utafiti katika Kituo cha Masomo ya Kiislamu, na alishiriki katika kuandaa ripoti za kisayansi zinazohusu masuala ya sasa katika fikra za kidini. Ana ujuzi wa lugha nne: Kiingereza, Kiarabu, Kirusi na Kifarsi, jambo lililompa uwezo wa kipekee wa kuwasiliana na wanafunzi kutoka asili tofauti.
Mbali na kumbi za masomo, Turambetov anapenda michezo, kucheza chess, kutatua mafumbo, kusoma vitabu, kuandika na kusafiri, mambo yote yanayoonyesha utu wake wa utulivu na upendo wake kwa maarifa na kugundua mambo mapya.
Hakika, wasifu wa Nurella Turambetov siyo tu safari ya kielimu, bali ni simulizi ya shauku juu ya ujumbe wa elimu na imani ya dhati kwamba kujenga binadamu ndilo njia fupi zaidi ya kujenga dunia yenye haki na amani zaidi.