Kusini dhidi ya Kusini: Kwa nini Afrika inashindwa kuugeuza umoja wake kuwa nguvu?

Kusini dhidi ya Kusini: Kwa nini Afrika inashindwa kuugeuza umoja wake kuwa nguvu?

Imeandikwa na: Dkt. Muhammad Ihsan
Chuo Kikuu cha Yale

Kuna janga la kipekee katika simulizi la Afrika ambalo haliwezi kuelezwa kikamilifu kwa ukoloni, uingiliaji wa nje, umaskini, au kushindwa kisiasa. Ni janga la bara limelozungumza tena na tena kwa lugha ya umoja, huku mara nyingi likitekeleza siasa za mgawanyiko. Kwa vizazi vingi, Afrika imekuwa ikikabiliana na dhuluma zilizotokana na nje, lakini baadhi ya changamoto zake zilizo na mizizi ya kina zaidi sasa zinaendelea kutokana na migongano iliyopo ndani ya bara lenyewe. Kusini imepambana dhidi ya Kaskazini, dhidi ya ukoloni, utegemezi wa kiuchumi, na mfumo wa kimataifa usio wa haki; lakini kuna mapambano mengine yanayostahili kupewa umakini zaidi: mapambano ya Kusini dhidi ya Kusini, mapambano ya nchi za Afrika dhidi ya nyingine, na mgongano kati ya maslahi ya kitaifa na ahadi pana zaidi ya mshikamano wa Afrika.

Afrika ya kisasa ilirithi mipaka ambayo kwa kiasi kikubwa ilichorwa bila ushiriki wa Waafrika; ambapo mamlaka za kikoloni ziligawa jamii, tamaduni, falme na mitandao ya biashara kwa kuzingatia maslahi yao wenyewe. Wakati wa kupata uhuru, viongozi wa Afrika walikabiliwa na chaguo gumu lisilo na suluhisho rahisi: kwani kuchora upya mipaka hiyo kulihatarisha kuzua migogoro ambayo ingeweza kuziteketeza nchi mpya zilizokuwa bado dhaifu. Kwa hiyo, ramani iliyorithiwa kwa kiasi kikubwa ilihifadhiwa. Hivyo, mkoloni aliondoka, lakini jiografia ya kisiasa ya kikoloni iliendelea kuwepo.

Hata hivyo, historia haiwezi kuwa maelezo ya kudumu ya hali ya Afrika ya sasa. Ukoloni ulitengeneza hali nyingi zinazoendelea kuathiri mwelekeo wa bara hili, lakini vizazi vilivyofuata pia vilifanya maamuzi yao wenyewe. Swali gumu sasa si tu kuhusu nani aliyechora mipaka ya Afrika, bali pia ni kwa nini mipaka hiyo bado inaendelea kubeba uzito mkubwa kiasi hiki wa kisiasa, wakati maslahi ya kiuchumi, kitamaduni na kiusalama ya jamii jirani yamefungamana kwa karibu.

Mkanganyiko huu unaonekana wazi katika mahusiano kati ya nchi za Afrika. Nchi ambazo zinategemeana katika biashara, usalama, nishati na upatikanaji wa masoko, mara nyingi hutenda kana kwamba ni washindani. Zinashindana katika ushawishi wa kikanda, uwekezaji, rasilimali, bandari na ushawishi wa kidiplomasia. Badala ya mipaka kurahisisha harakati za biashara, hugeuka kuwa vikwazo, huku tofauti za kisiasa kati ya serikali zikiwa na uwezo wa kuvuruga maisha ya wananchi wa kawaida ambao hawahusiki kwa namna yoyote na migogoro hiyo.

Hili ndilo eneo kuu la udhaifu katika ujumuishaji wa Afrika: umoja huadhimishwa kama lengo la kimawazo, lakini ushirikiano huwa mgumu pale unapohitaji serikali kufanya makubaliano yanayogusa maslahi yao ya kitaifa ya moja kwa moja. Ujumuishaji wa kweli unahitaji uaminifu; unahitaji nchi kubwa kudhibiti ushawishi wao, nchi ndogo kukubali kanuni ya kutegemeana, na serikali kutambua kwamba ustawi wa nchi jirani si lazima upunguze ustawi wao wenyewe.

Changamoto za kiusalama barani Afrika zinafanya kushindwa huku kuwa na gharama kubwa zaidi. Ugaidi, uhalifu uliopangwa, usafirishaji haramu wa silaha, uhamiaji na ukosefu wa utulivu wa kisiasa ni masuala ambayo hayaheshimu mipaka ya kitaifa, lakini bado majibu yake kwa kiasi kikubwa yanaendelea kuwa ya kitaifa. Mgogoro katika nchi moja unaweza kuvuruga utulivu wa nchi nyingine kadhaa, huku hali ya kutoaminiana ikizifanya serikali kutafsiri hatua za kujilinda za majirani zao kama vitisho. Matokeo yake ni mzunguko ambapo ukosefu wa usalama huzalisha mashaka, mashaka huzalisha ushindani, na ushindani hufanya ushirikiano wa kweli katika masuala ya usalama kuwa mgumu zaidi.

Tatizo hilo hilo linaonekana katika usimamizi wa utajiri mkubwa wa asili ambao Afrika imejaaliwa. Bara hili lina rasilimali nyingi za madini, kilimo na nishati, lakini mara nyingi wingi wa rasilimali umeenda sambamba na umaskini na utegemezi.
Bila shaka, unyonyaji wa nje ni sehemu ya historia hii, lakini Afrika pia inapaswa kukabiliana na mgawanyiko wake yenyewe. Bara linalojadiliana kwa kutengana kuhusu uwekezaji, teknolojia, miundombinu na upatikanaji wa masoko, lina uwezo mdogo zaidi wa kujadiliana kuliko bara linaloweza kuratibu maslahi yake.

Kwa hiyo, tatizo la Afrika si ukosefu wa rasilimali pekee, bali ni kushindwa kwa kuendelea kubadilisha rasilimali za pamoja kuwa nguvu ya pamoja.

Hili ndilo hasa lililokuwa jambo la kuwahofia waanzilishi wa fikra za umoja wa Afrika katika hatua zake za mwanzo. Viongozi kama Kwame Nkrumah walitambua kwamba uhuru wa kisiasa, bila ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa, unaweza kuziacha nchi za Afrika zikiwa na mamlaka rasmi ya kujitawala, lakini zikiwa bado katika hali ya udhaifu wa kimkakati. Hata hivyo, mradi wa umoja wa Afrika umekabiliwa mara kwa mara na mvutano kati ya mamlaka ya kitaifa na ujumuishaji wa bara. Inaeleweka kwamba serikali zilinde uhuru wao, hasa kwa kuzingatia historia ya Afrika ya kutawaliwa na nguvu za nje. Lakini mamlaka ya kujitawala hayapaswi kuchanganywa na kujitenga. Katika dunia inayotegemeana, hatua za pamoja zinaweza kuimarisha nguvu ya kitaifa badala ya kuipunguza.

Nchi inayojadiliana peke yake na dola kubwa ya kimataifa huwa na ushawishi mdogo, wakati soko la kikanda lililoratibiwa, linalojumuisha mamia ya mamilioni ya watu, huwa na ushawishi mkubwa zaidi. Nchi inayojadiliana peke yake kuhusu rasilimali za kimkakati huwa na msimamo mmoja wa majadiliano, wakati nchi kadhaa zinazofanya kazi kwa pamoja huwa na msimamo tofauti. Kwa hiyo, ujumuishaji si kuachia mamlaka ya kujitawala, bali ni —ikiwa utaundwa kwa usahihi— njia ya kuimarisha na kuongeza mamlaka hiyo.

Nguvu za nje pia zimenufaika kutokana na migawanyiko ya Afrika, na ni jambo lisilo na busara kupuuza ukweli huu. Serikali na makampuni ya kigeni kihistoria yametumia ushindani wa kisiasa na kufuatilia maslahi yao ya kimkakati katika bara zima. Hata hivyo, kwa wahusika wa nje ni rahisi zaidi kutumia migawanyiko iliyopo kuliko kuunda umoja wa kweli. Kwa hiyo, Afrika inapaswa kupinga mwelekeo wa kueleza kila kushindwa kwake kwa kuhusisha na uingiliaji wa nje. Unyonyaji wa nje ni ukweli unaoonekana, lakini utashi na uwezo wa Waafrika wa kuchukua hatua kwa niaba yao wenyewe pia ni ukweli halisi wenye uzito sawa.

Gharama kubwa zaidi ya mgawanyiko huu hulipwa na wananchi wa kawaida wa Afrika. Mipaka inapofungwa, wafanyabiashara hupoteza mapato na riziki zao; miradi ya kikanda inapokwama, kampuni hupoteza masoko yake; na migogoro ya kisiasa inapozuia usafirishaji na uhamaji, familia na jamii huathirika. Kwa Mwafrika wa kawaida, mgawanyiko si tatizo la kidiplomasia la kinadharia tu, bali ni mpaka uliofungwa, safari ya gharama kubwa, kizuizi cha forodha, fursa iliyopotea, au kikwazo cha kiurasimu kinachosimama kati ya watu ambao, bila vikwazo hivyo, wangeweza kufanya biashara, kufanya kazi na kuishi kwa urahisi katika maeneo yaliyo ng’ambo ya mipaka.

Afrika haihitaji tangazo jingine la umoja, bali inahitaji kuufanya umoja huo kuwa jambo la vitendo. Inahitaji miundombinu iliyounganishwa, biashara iliyo huru zaidi, usalama ulioratibiwa, taasisi za kikanda zilizo imara zaidi, na viongozi wa kisiasa walio tayari kukubali kwamba ushirikiano wakati mwingine huhitaji kufanya makubaliano na kutoa baadhi ya maslahi ya kitaifa. Zaidi ya yote, inahitaji kuachana na dhana kwamba maendeleo ya kitaifa lazima yaje kwa gharama ya nchi jirani.

Afrika haihitaji kuwa taifa moja ili iwe nguvu moja. Nchi zake zinaweza kuhifadhi utambulisho na mamlaka yake ya kujitawala, huku zikitambua wakati huo huo kwamba faida yake kubwa ya kimkakati iko katika uzito wa nguvu zake za pamoja.

Mapambano ya Kusini dhidi ya Kusini hatimaye ni mapambano kuhusu ikiwa Afrika inaweza kugeuza jiografia yake ya pamoja kuwa nguvu ya pamoja. Ukoloni unaeleza mengi kuhusu historia ya bara hili, lakini hauwezi kuamua mustakabali wake milele. Uingiliaji wa nje ni ukweli unaokuwepo, lakini hauwezi kuwa kisingizio cha mgawanyiko wa ndani usio na mwisho.Mamlaka ya kitaifa ya kujitawala ni jambo la msingi, lakini hayapaswi kugeuzwa kuwa kisingizio cha kuendelea kugawanyika daima.

Kwa vizazi vingi, Afrika imekuwa ikiuliza kwa nini dunia inaendelea kuigawa. Labda sasa umefika wakati wa kuuliza swali gumu zaidi: Kwa nini Afrika inaendelea kuruhusu migawanyiko hiyo kupunguza nguvu yake?

Jibu halitapatikana katika hotuba nyingine kuhusu udugu, bali litapatikana katika kazi ngumu ya kujenga uaminifu, kuunganisha uchumi, kuimarisha taasisi, na kujifunza kuutazama ushirikiano si kama makubaliano ya kuwanufaisha nchi jirani kwa gharama ya wengine, bali kama uwekezaji katika Afrika yenyewe.

Mustakabali wa Afrika hautaamuliwa tu na kile ambacho dunia inafanya kwa Afrika, bali pia utaamuliwa na kile ambacho Afrika itachagua kujifanyia yenyewe.